WACHEZAJI wapya wa Simba, kipa Yakoub Suleiman na beki wa kati Wilson Nangu tayari wamepigwa picha zitakazotumika kuwatangaza kuwa sehemu ya kikosi hicho kwa msimu ujao.
Chanzo cha uhakika cha Mwanaspoti kimesema baada ya Simba kukamilisha kila kitu kwa ajili ya usajili wa wachezaji hao, leo Jumanne wamepigwa picha kabla ya kujiunga na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayojiandaa kucheza michuano ya kufuzu za Kombe la Dunia 2026.
Nangu aliyemaliza Ligi Kuu Bara msimu uliopita akiwa amefunga mabao mawili, asisti mbili ilhali Yakoub akiwa na ‘clean sheet’ nane kila mmoja amesaini Simba mkataba wa miaka mitatu.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa Simba ilitoa Sh 400 milioni kuwanasa wachezaji hao kutoka JKT Tanzania nje na dau lao binafsi pamoja na Sh50 milioni ilizotoa kwa JKU kama mwajiri wa Yakoub.
“Tayari wamepigwa picha na Simba, hivyo wanaweza wakatangazwa muda wowote kuanzia sasa kwa mashabiki ambao tunawaomba wawape ushirikiano wa kuwasapoti,” kimesema chanzo hicho na kuongeza:
“Nangu atawaongezea nguvu kina Abdulrazack Mohammed Hamza na Chamou Karabou wakati Yakoub atakuwa mbadala wa Ally Salim anayetarajia kumalizana na Simba kutokana na mkataba wake wa miaka mitatu uliosalia.”