LICHA ya kutoshiriki fainali za Cecafa Kagame 2025, Simba inashikilia rekodi mbili kwa wakati mmoja ikiwa ni timu iliyotwaa mataji mengi zaidi na ndiyo iliyopoteza mechi nyingi zaidi za fainali katika mashindano hayo.
Wekundu hao wa Msimbazi wametwaa taji mara sita miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002 na kuwafanya kuwa timu yenye historia ndefu ya mafanikio katika mashindano hayo.
Hata hivyo, upande mwingine wa sarafu unaonyesha taswira ya machungu. Simba imepoteza fainali saba – zaidi ya timu nyingine yoyote ikiwemo moja wakati huo ikiitwa Sunderland.
Mara ya kwanza Simba kupoteza fainali ilikuwa 1967 mbele ya AFC Leopards ya Kenya ambayo wakati huo ilitambulika kama Abaluhya kwa mabao 5-0, ikapoteza tena 1975 ilipokabwa na Yanga. Baada ya hapo, iliendelea kupoteza mechi muhimu, 1978 ikapigwa na Kampala City Council, 1981 ikazimwa na Gor Mahia, 2003 ikapoteza kwa Villa, 2011 ikafungwa na Yanga, 2018 ikapoteza kwa mara ya mwisho mbele ya Azam kwa mabao 2-1.
Kwa jumla, Simba SC imefika fainali 13 katika historia ya mashindano hayo.
Hii ni idadi kubwa zaidi kuliko timu nyingine yoyote, jambo linaloonyesha uthabiti na uwezo wao wa kila wakati kufika hatua za juu.
Historia hii inatofautisha Simba na timu nyingine za ukanda wa Cecafa. Timu kama SC Villa ya Uganda na APR FC ya Rwanda pia zimepoteza fainali mara kadhaa, lakini Simba ndio inayoshika rekodi ya kupoteza fainali mara nyingi zaidi na kushinda mataji mengi zaidi ya mashindano hayo.