Tabora United yatangulia nusu fainali kwa kishindo

USHINDI wa mabao 4-0 ilioupata Tabora United dhidi ya Eagle FC, umeifanya timu hiyo kufuzu nusu fainali ya mashindano ya Tanzanite Pre-Season International.

Tabora United imetinga nusu fainali kufuatia kukusanya pointi sita kwenye Kundi A lenye timu tatu baada ya kushinda mechi zote mbili.

Katika mchezo uliofanyika leo Septemba 2, 2025 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, Chewe Chanda alianza kuifungia Tabora United dakika ya 23.

Kabla ya kuingia kwa bao hilo, Eagle FC ilitengeneza nafasi tatu za wazi, lakini wachezaji wa timu hiyo, Maliki Saidi na Ally Rajab walikosa utulivu na kushindwa kufunga.

Dakika ya 33, Joseph Akandwanaho akafunga bao la pili likiwa pia la pili kwake katika mashindano hayo ambapo pia alifunga mchezo wa kwanza dhidi ya Fountain Gate.

Kipindi cha kwanza kilimalizika Tabora United ikiwa mbele kwa mabao 2-0 huku ikiwa imechonga vizuri barabara ya kutinga nusu fainali.

Adam Omary Adam, akaongeza bao la tatu dakika ya 53, kisha Ramadhan Chobwedo akahitimisha ushindi dakika ya 57, likiwa pia ni bao lake la pili la mashindano.

Hata hivyo, Tabora United ilimaliza pungufu ya mchezaji mmoja baada ya Ibrahim Mahamane kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 85 kutokana kumchezea faulo Abdul Maro nje kidogo na eneo la hatari.

Mashindano ya Tanzanite Pre-Season International yanayofanyika kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, yakiandaliwa na Fountain Gate FC, yalianza Agosti 31, 2025 na tamati yake ni Septemba 7, 2025 ambapo utapigwa mchezo wa fainali. Kabla ya hapo, Septemba 6, zitachezwa mechi za nusu fainali.

Jumla ya timu 10 zinashiriki zikiwa zimepangwa katika makundi matatu. Kundi A lina timu za Fountain Gate, Tabora United na Eagle FC ya Manyara.

Kundi B zipo Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Coastal Union, huku Kundi C kuna Namungo, JKU ya Zanzibar, City Abuja (Nigeria) na TDS inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwa inaibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi.