Tishio jipya wizi mita, koki za maji

Dar es Salaam. Wimbi la wizi wa mita na koki za maji limezidi kuwa kero, likiathiri upatikanaji wa huduma kwa mamia ya wananchi na kusababisha upotevu mkubwa wa mapato kwa mamlaka za maji.

Uhalifu huo unatajwa kuchangiwa na wauza vyuma chakavu na mafundi wanaotengeneza mapambo au vifaa vya matumizi ya nyumbani kwa kutumia miundombinu hiyo ya maji.

Mmoja wa mafundi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) aliyeomba hifadhi ya jina ameiambia Mwananchi kwamba wezi wanalenga kuuza vyuma vilivyopo ndani ya mita hizo na pia kutengeneza mapambo ya urembo kama vile bangili.

Akizungumza leo Jumanne Septemba 2, 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri alipoulizwa kuhusu wizi huo, alikiri kuwapo akibainisha wizara imeanza kuchukua hatua kukabiliana nao.

“Siyo wizara ya maji tu, mfano hata kwenye barabara kuna watu walikuwa wakiiba nguzo za barabarani, ukienda Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) watu walikuwa wakiiba zile nyaya za copper (shaba), kwenye majitaka waliiba mifuniko,” amesema na kuongeza:

“Tukija kwenye mita, hayo yanatokana na sababu ya teknolojia, tatizo linapotokea ndipo mnajua namna ya kukabiliana nalo.”

Amesema kutokana na changamoto hizo, wanaangalia kitu kinachoibwa kinachukuliwa kwa sababu gani.

“Tunabadilika kulingana na changamoto, kama mita za plastiki hakuna any issue (tatizo), zile zinazoibwa waliona humo ndani kuna material (malighafi) wameyaona yana thamani, changamoto hizo zipo maeneo mengi,” amesema.

Kuhusu utaratibu wa kurejesha mita kwa wateja ambao wameibiwa, Mwajuma amesema kila mamlaka ina utaratibu wake.

“Huko ndipo watakuwa na majibu sahihi kueleza wana deal (shughulikia) nazo vipi, maana kuna wengine wamekamatwa na kesi zinaendelea, hivyo mamlaka za mikoa husika zina utaratibu na majibu sahihi,” amesema.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasilino cha Dawasa, Everlasting Lyaro alipoulizwa amesema wameanza kulifanyia kazi na watakapokamilisha taratibu zote watatoa taarifa.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (Suwasa), kupitia Ofisi ya Mawasiliano na Uhusiano wa Umma, Julai 26, 2025 kwenye tovuti yake ilitoa onyo kwa wananchi wanaojihusisha na vitendo vya wizi wa miundombinu ya maji, zikiwamo mita, koki na vifaa vingine vinavyohusiana na usambazaji wa maji.

Pia, ilitoa onyo kwa wauza vyuma chakavu na mafundi wanaotengeneza mapambo au vifaa vya matumizi ya nyumbani kwa kutumia miundombinu hiyo ya maji.

Suwasa ilisema atakayefanikisha kutoa taarifa sahihi itakayowezesha kukamatwa kwa wezi wa miundombinu ya maji atajipatia zawadi ya Sh500,000.

Julai 23, 2025, Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama (Kuwasa), John Mkama alikaririwa na vyombo vya habari akieleza mita za maji 542 zimeripotiwa kuibwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.

Alisema matukio ya wizi wa mita za maji yameshamiri katika kata za Nyahanga, Malunga, Majengo na Mhongolo, hali inayosababisha wananchi kukosa maji. Aliwaomba wananchi kushirikiana na mamlaka ili kuwabaini wezi hao, akieleza wanashirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwasaka.

Clara Joseph mkazi wa Kibamba, wilayani Ubungo ni miongoni mwa walioibiwa mita, amesema iliibwa mchana.

“Niliamka asubuhi nikatumia maji kutoka bombani. Saa 2:30 asubuhi niliondoka nyumbani nikaacha mita ipo. Mchana saa nane nilishtushwa na simu ya jirani yangu kuwa mita haipo,” amesema Clara ambaye ni miongoni mwa mamia ya wananchi walioathiriwa na wizi huo.

Elisante Yona, mkazi wa Kibaha mkoani Pwani amesema mita yake iliibwa Julai 6, 2025 na tangu wakati huo anahangaika kupata nyingine.

“Niliripoti Dawasa wakaja kufunga maji, nilitakiwa nilipie Sh50,000 kwa ajili ya kupata mita nyingine, nikafanya hivyo, lakini hadi leo sijapata mita mpya. Nalazimika kuingia gharama ya kununua maji ya madumu,” amesema.

Kupitia kundi sogozi la Whatsapp la huduma kwa wateja la Dawasa Kibamba, kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wateja kuhusu wizi wa mita na koki.

“Haipiti wiki mita kwenye eneo letu haijaibwa, tunashangaa ni kwa nini hali hii? Zamani haya mambo hayakuwepo, kuna kitu gani hivi sasa kwenye hizi mita?” amehoji na kuongeza:

“Sioni ufuatiliaji wa kina wa Dawasa kwenye hili, kinachofanyika ni kama kuweka hela kwenye mifuko iliyotoboka.”

Baada ya mteja kubaini mita yake imeibwa, anapaswa kwenda kupata taarifa ya Jeshi la Polisi kuhusu upotevu wa mali, ambayo ili kuipata ni lazima kuilipia kutoka kwa watoa huduma kwenye ‘steshenari’ baadhi wakitoza Sh5,000.

Baada ya kuifikisha taarifa hiyo Dawasa, mteja anapaswa kuandika barua kuomba kupatiwa mita mpya kisha atapatiwa namba ya malipo ili kulipia Sh50,000.

Baada ya kukamilisha malipo, atapaswa kusubiri hadi mwezi mmoja kabla ya kupatiwa mita mpya, hivyo kupata adha ya kutafuta mbadala wa huduma ya maji.

“Ni usumbufu kwa kweli, kwanza utatakiwa uilipie hiyo mita Sh50,000, kisha uanze kusubiri kufuatilia ni lini utaletewa mita nyingine, inachukua muda mrefu. Dawasa itusaidie katika hili, hatujui nini kimewekwa kwenye hizi mita hadi ziwe zinaibwa namna hii? Tumechoka kuibiwa mita na kutakiwa tulipie tena ili kuzipata kwa usumbufu na pesa nyingine zinatoka wapi?” amehoji mteja aliyeibiwa mita.

Mteja mwingine mkazi wa Kimara Suka, Dar es Salaam, Nelia Elisha amesema: “Hizi mita zinaibwa kila leo, tulitamani Dawasa watuambie nini cha kufanya, lakini inapotokea umeibiwa watakwambia nenda polisi, ukifuata utaratibu wao na kulipia, mita mpya inakuja kufungwa palepale, nini maana yake?” amehoji.

Amesema inaumiza kutoa fedha ambayo haukuitarajia na kuongeza: “Tulishafanya jitihada tukaweka maji, hizi mita hazikai ndani, ziko nje na huwezi kusema nikae usiku kucha kuilinda, katika huu wizi tunaomba Serikali ituangalie, yenyewe ndiyo inatakiwa kuwajibika.”

Baadhi ya wateja wamejikuta wakitumia maji nje ya mfumo wa Dawasa kwa kuibwa mita, hali inayosababisha mamlaka kukosa mapato na pia kuwaweka katika hatari ya kushtakiwa kwa wizi wa maji watakaobainika.

Wengine hulazimika kukunja mipira ya maji ili yasiendelee kumwagika baada ya mita kuibwa.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizindua taarifa ya utendaji wa mamlaka za maji kwa mwaka 2023/24 Machi 19, 2025 jijini Dar es Salaam alizielekeza mamlaka za maji kupunguza kiwango cha upotevu maji ili kuepusha hasara ya Sh114.12 bilioni iliyotokana na upotevu huo kwa mwaka huo.