BAADA ya Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya ndani (CHAN 2024) kumalizika, wadau mbalimbali wametoa mtazamo wao ya kujifunza kwa ajili ya AFCON 2027, itakayohusisha nchi tatu mwenyeji za Tanzania, Kenya na Uganda.
Hatua ya mitazamo hiyo imekuja baada ya nchi hizo tatu kupewa uenyeji kuandaa tena michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, huku wadau mbalimbali wa soka wakieleza mambo ya kuzingatia na changamoto mbalimbali za kukabiliana nazo.
Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah amesema licha ya mafanikio yaliyopatika kwa ujumla katika CHAN 2024, ila kuna jambo la kujifunza ambalo ni namna Ofisa Masoko wa mtandaoni kuhamasisha mashabiki.
“Kuna namna ya kuwaelimisha mashabiki kununua tiketi mitandaoni ambalo ni eneo la Ofisa Masoko mtandaoni, ndio maana nasisitiza eneo hilo, wenzetu Kenya wamefanya vizuri ndiyo maana mashabiki walikuwa wanajaa uwanjani,” amesema Angetile.
Angetile amesema endapo zamani wangekuwa wanafanya michuano hiyo kwa kanda (zone) basi Taifa Stars ingeshiriki mara nyingi zaidi, kwani anafikiri tukirudi kwa mtindo huo utatoa picha halisi ya kushindana na timu ngumu tofauti na sasa.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amesema nchi ijaribu kutengeneza mazingira rafiki kwa wageni kuingia kwa urahisi, pia urahisi wa watu kuingia uwanjani, kwani kuna mataifa wanafunga hadi barabara zao.
“Kuna mataifa wanafunga barabara ili kurahisisha watu waende kirahisi uwanjani, lengo ni kupunguza adha ya usafiri, pia kuongeza hamasa kwa watu kuingia uwanjani, kuna timu inaitwa unaona imetokea kwa sababu mtu fulani hayupo,” amesema.
Aidha Zaka amesema, licha ya kuandaa mashindano makubwa ila kama nchi hatujanufaika na chochote katika suala nzima la miundombinu, kutokana na kuchezwa kwenye uwanja ambao ulikuwepo na haujajengwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji husika.
Mhariri wa Masuala ya Uchumi wa Gazeti la Mwananchi, Ephrahim Bahemu, amesema mafanikio makubwa ya kujivunia kwa CHAN 2024 ni ya timu zote tatu, kwani yameongeza ubora, licha kuandaa kwa mara ya kwanza kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki.
“Kiuchumi tumefanikiwa kupata wageni wengi sekta za kiuchumi zimepata chochote kitu, timu zililala katika mahoteli na fedha za kigeni pia tunaweza kuhesabu kama manufaa, wachezaji wameongeza pia uzoefu kwa kukutana na nchi bora zaidi.”
Mwandishi mwandamizi wa habari za michezo kutoka Kampuni ya Mwananchi Communications, Charles Abel amesema Kwa namna ya CHAN 2024, ilivyopewa sapoti katika mitandao ya kijamii yalikuwa na mvuto kwa nchi wenyeji za Tanzania, Kenya na Uganda.
“Changamoto ilikuwa ni namba ndogo ya mashabiki kwa upande wetu Tanzania, ukilinganisha na wenzetu Kenya na Uganda, hili ni jambo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi katika Michuano ijayo ya AFCON 2027, tukakayoshirikiana pamoja,” amesema Abel.
Mwandishi wa habari wa Uganda, David Isabirye wa Kawowo Sports amesema Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN 2024) iliyofanyika kwa maandalizi ya pamoja nchi za Uganda, Kenya na Tanzania ilikuwa na mafanikio makubwa.
“Haya mashindano tujipongeze kwa mataifa yote matatu, tumeonyesha ushirikiano mkubwa, Unapoona marais wa CAF, Patrice Motsepe na Gianni Infantino wa FIFA, wakipongeza maandalizi, hii ni hatua kubwa kwetu kwenye fainali za Mataifa za mwaka 2027.”
Isabirye amesema, licha ya Uganda kuanza taratibu michuano ya CHAN 2024, ila wamefanya vizuri hadi kufika robo fainali, huku akivutiwa na timu zote mwenyeji zilizoandaa, kutokana na kuonyesha ushindani mkubwa kuanzia mwanzoni ilipoanza.
Mwandishi mwandamizi wa habari za michezo kutoka Kampuni ya Mwananchi Communications, Khatimu Naheka, amewapongeza waandaaji wa Michuano ya CHAN kwa kuimarisha ulinzi na kuonyesha soka linavyoweza kuwaweka watu na kusahau mambo ya siasa.
“Waandaji wamefanya vizuri kwa kuandaa na kuweka ulinzi ulikuwa mkubwa, kilichokuwa kikionekana Kenya kwa watu kutokea kwa wingi uwanjani kwa furaha bila vurugu, imeonyesha namna ambavyo soka linasahaulisha mambo ya kisiasa na kutengeneza umoja.”
Kwa upande wa Mwandishi wa Habari wa Ghana Soccernet, Nuhu Adam amesema michuano hiyo, ndio bora zaidi kwake tangu imeanza rasmi mwaka 2009.
“Hii ni hatua nzuri kwa nchi zote tatu ambazo zimeandaa michuano hii, nafikiri kwangu ndiyo mashindano bora zaidi kuwahi kutokea, CAF ilifanya kazi yake vizuri kwa kushirikiana na wenyeji, hivyo kiukweli ni jambo la kuvutia,” amesema Nuhu.
Nuhu amesema sababu ya Shirikisho la Soka Africa (CAF), kuanzisha CHAN ni dalili nzuri ya kuandaa vizuri timu zote za ukanda wa Afrika kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya AFCON, ambayo ndio mikubwa zaidi kutokana na aina ya wachezaji.
“Siwezi kuzungumzia kasoro kwa sababu yapo mambo mengi yamefanyika kwa soka la Afrika Mashariki, timu kama Yanga, Simba kwa Tanzania, Gor Mahia ya Kenya zinafanya vizuri pia, hii ni dalili tosha ya jinsi nchi hizo tatu zilivyopiga hatua.”
Aidha, Nuhu amesema licha ya maandalizi bora kwa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ila zinapaswa kuendelea kujiimarisha vizuri katika michuano ya Mataifa ya Afrika AFCON 2027, ambayo inahusisha nyota wengi wakubwa kutoka mataifa mbalimbali.