Abiria treni ya Ubungo walalamikia ubovu wa reli, giza usiku, kung’atwa na mbu

Dar es Salaam. Abiria wanaotumia treni ya Kariakoo kwenda Ubungo maarufu kama Treni ya Mwakyembe wamelalamikia ubovu wa kipande cha reli kutoka Barabara ya Mandela hadi Kwa Mnyamani, Buguruni, hali inayowafanya kurushwarushwa na kugongana wakati wa safari.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti, abiria hao wameiomba TRC kuitupia jicho reli hiyo kabla haijasababisha maafa.

Pia wamedai kuwa baadhi ya wahudumu wa treni inapofanya safari ya mwisho kutoka Ubungo kwenda Kamata, hushuka njiani huku wakifunga vioo na kuzima taa, jambo linalowafanya abiria kukosa hewa na kuumwa na mbu.

Uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) umesema umeyasikia malalamiko hayo kwa mara ya kwanza na umeahidi kuyafanyia kazi.

Akizungumzia malalamiko hayo, Msemaji wa TRC, Fred Mwanjala, alisema: “Niseme tumepokea malalamiko hayo ya wananchi, tulikuwa hatulijui hilo, niwaahidi kwamba tunalifanyia kazi na hivi karibuni wataona mabadiliko.”

Eneo la Mnyamani ambapo treni ya Ubungo husimama kwa muda  kupisha  treni ya Pugu ipite

Monica David, mkazi wa Mabibo, alisema kurushwarushwa huanzia pale Mwananchi hadi Kwa Mnyamani, Buguruni, na hali huwa tete kiasi kwamba abiria huogopa kusafiri.

“Yaani hiki kipande Mungu tu ndiye anatusaidia, kwani unarushwarushwa kama mtu anayepita barabara yenye mashimo, wakati tunajua reli ni mtelezo. Hadi unajiuliza hivi reli nayo siku hizi ina mashimo? Hebu mamlaka ilifanyie kazi hili, sio isubiri maafa yatokee ndipo waanze kukimbizana,” alisema Monica.

Alphonce Tarimo, mkazi wa Ubungo Maziwa, alisema kutokana na mtikisiko huo wakati mwingine abiria hugongana wakiwa wamekaa, na kwamba behewa la mwisho ndilo huathirika zaidi.

Mbali na hayo, alisema milango ya kuingia na kutoka abiria imekuwa ikijifunga na kufunguka kwa nguvu, hali inayotishia kuharibika na pia imesababisha kelele.

Josephine Mlilo, mkazi wa Tabata Kisiwani, amesema alipokuwa mjamzito alilazimika kushukia kituo cha Mnyamani baada ya kupandia Tabata Mwananchi kutokana na mtikisiko mkubwa.
“Hali niliyokuwa naisikia wakati napanda treni hiyo nikiwa naenda kliniki, malaika wangu ndio walijua. Kwa ule mtikisiko niliona kama naenda kuzaa kabla ya wakati, na tangu siku hiyo sijarudia kuipanda tena licha ya kuwa ilinisaidia kuwahi mjini,” alisema Josephine.

Amani John, mkazi wa Mbagala, alisema huipenda treni hiyo kwa kuwa humsaidia kuepuka foleni kubwa ya Buguruni, ingawa amekuwa akisafiri “roho mkononi.”
“Huwa nikipanda Tabata Mwananchi nashuka Bakhresa, kisha nachukua bajaji kwenda Mbagala na hivyo kuokoa muda. Lakini kila safari najiuliza, kweli mafundi wa TRL hawalioni hili au wamezoea?” alisema John.

Ashery Gustav, mfanyabiashara wa Kariakoo, alisema mbali na ubovu wa reli, hata treni yenyewe imeonekana kutelekezwa.
“Ifike mahali hii treni ikarabatiwe. Hata kama ni usafiri wa umma bado unatakiwa kuwa katika hali nzuri ya muonekano.

“Pia inaweza kuvutia wafanyabiashara kutangaza kupitia treni hii kwa kuwa ni bango linalotembea, na hivyo kuingizia shirika mapato badala ya kutegemea nauli pekee,” alisema Gustav.