Adam apigia hesabu mpya Tabora United

MSHAMBULIAJI wa Tabora United, Adam Adam amesema mashindano ya Tanzanite Pre-Season International Tournament yaliyoandaliwa na Fountain Gate na kufanyika kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara, yanawasaidia kuwaweka tayari kimwili na kimbinu kwa ajili ya hesabu mpya za msimu wa Ligi Kuu Bara inayotarajia kuanza Septemba 17.

Nyota huyo wa zamani wa Azam, Tanzania Prisons, KMC na Mashujaa ameliambia Mwanaspoti namna mashindano hayo yanavyowajenga kutokana na kucheza na timu za Ligi Kuu, zinazowaweka sawa kiushindani kutokana na majukumu yaliyopo mbele yao.

Adam katika msimu wa 2023/24 alimaliza na mabao saba akiwa Mashujaa kisha kujiunga na Azam msimu uliopita kwa mkataba wa mwaka mmoja, kabla ya kutolewa kwa mkopo kwenda Tanzania Prisons, alisema matarajio yake ligi ya 2025/26 ni kujituma kwa bidii, ili awe katika orodha ya wachezaji wanaotajwa kufunga mabao mengi.

“Mashindano yaliyoandaliwa na FG ni mazuri sana, tunakutana na timu za kiwango chetu, hivyo tutakapoanza ligi tutakuwa tunajiamini vya kutosha, kwani tumepimwa kwa kipimo sahihi,” alisema Adam na kuongeza; “Hadi tutakapomaliza hayo mashindano tutaondoka na kitu kikubwa sana.”