ANGELLAH KAIRUKI: “NITAENDELEZA KASI, HAKUNA MRADI UTAKAOSIMAMA KIBAMBA”

Kibamba, Dar es Salaam – Mgombea ubunge wa Jimbo la Kibamba
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Angellah Kairuki, ameendelea na ziara yake
ya kampeni kwa lengo la kuimarisha mshikamano na mshikikiano miongoni mwa
wanachama wa chama hicho.

Katika ziara hiyo, Kairuki alibainisha kuwa moja ya
vipaumbele vyake ni kuhakikisha changamoto za wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa
kudumu. Alitaja changamoto za soko, maeneo ya kuzikia pamoja na barabara kuwa
ndizo zinazowakabili wakazi wengi wa Kibamba.

“Nitaendeleza kasi tuliyoanza, hakuna mradi wowote
utakaosimama. Nitahakikisha wananchi wa Kibamba wananufaika na maendeleo ya
kweli,” alisema Kairuki.

Amesisitiza kuwa dhamira yake kubwa ni kuwalipa wananchi kwa
uwajibikaji, kusikiliza sauti zao na kuwapigania ili jimbo la Kibamba liendelee
kusonga mbele.

Kwa mujibu wake, mshikamano wa wanachama wa CCM katika jimbo
hilo ndiyo chachu ya ushindi na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo
inayotarajiwa kuinua maisha ya wananchi.