MIAMBA ya soka la Rwanda, APR itatupa karata yao ya kwanza leo, Jumatano kwenye mashindano ya Kombe la CACAFA Kagame 2025 ambayo yalianza jana,Jumanne kwa kucheza dhidi ya Bumamuru FC ya Burundi huku ikiwa na hesabu ya kutwaa kombe hilo kwa mara ya nne.
APR ni miongoni mwa klabu zilizofanikiwa zaidi kwenye Ligi ya Rwanda baada ya kutwaa mataji 22 na Kombe la Rwanda mara 13 huku 2022, ikifikia raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) kwa mara ya kwanza katika historia yake.
Bumamuru FC yenyewe ni klabu changa ukilinganisha na APR kutokana na kuanzishwa kwake miaka 11 iliyopita, lakini imekuwa moja ya timu ambazo zinafanta vizuri kwenye ligi ya Burundi.
Mbali na msimu uliopita APR kupoteza fainali ya michuano hii ya Kombe la CECAFA Kagame mbele ya Red Arrows kwa mikwaju ya penalti, timu hiyo ina historia ya kutwaa taji hilo mara tatu. Ilifanya hivyo mwaka 2004, 2007 na 2010, baada ya kufika fainali na kupoteza mwaka 1996 na 2000.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizi kukutana katika mashindano haya ambayo yalianza mwaka 1967 ambapo timu iliyofahamika kama Abaluhya kwa mujibu wa Wikipedia ilitwaa ubingwa, lakini hayakutambuliwa rasmi. Mashindano hayo yalisimama hadi 1974, ambapo Simba ikawa mabingwa wa kwanza kutambuliwa rasmi.
Kocha wa zamani wa timu ya taifa la Tanzania na klabu ya Yanga, Márcio Máximo naye atakuwa kibaruani kuiongoza KMC katika mchezo wake wa kwanza wa ushindani dhidi ya Mlandege kwenye Kombe la CECAFA Kagame.
Akizungumzia mechi hiyo ya pili kuchezwa leo baada ya ile ya mapema kati ya APR dhidi ya Bumamuru FC, Maximo alisema: “Itakuwa mechi ngumu lakini tumejiandaa vizuri, naamini tutafanya vizuri na mashindano haya yatatupa maandalizi mazuri kuelekea msimu ujao.”
Kabla ya mashindano haya, KMC iliweka kambi Zanzibar na kucheza mechi za kirafiki ikiwemo dhidi ya KMKM na kutoka sare ya bao 1-1, hivyo kocha huyo atakuwa anajua namna ya kukabiliana na timu kutoka visiwano humo kwa Mlandege hii itakuwa ni nafasi ya kuonyesha ubabe wake dhidi ya timu ya Tanzania Bara.
Mlandege sio timu ya kubezwa inahistoria kubwa katika mashindano hayo kuliko KMC, 1998 ilicheza fainali ya Kombe la CECAFA Kagame na kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda.