Bado Watatu – 17


“HEBU eleza tukio lilivyotokea.”

Akaniambia kwamba yeye alikuwa muuguzi wa hospitali ya Bombo ambayo ni ya mkoa. Jana yake alikuwa na zamu ya kulala kazini. Lakini aliporudi asubuhi kutoka kazini akakuta wezi wameruka ukuta na kuvunja mlango wa nyuma na kumuibia vitu kadhaa.

“Unasema waliruka ukuta wakavunja mlango wa nyuma?”

“Ndiyo.”

“Wameiba nini?”

“Labda niseme wamenisafisha. Wameiba majiko, feni, televisheni yangu, sabufa. Magodoro na pesa taslimu shilingi laki sita zilizokuwa kwenye kabati.”

Baada ya kuandika vitu vilivyoibwa nilimuuliza Hamisa: “Vitu hivyo vyote vina thamani gani?”

“Karibu milioni nne.”

“Pole sana. Kuna watu wowote ambao unawashuku?”

“Wapo.”

“Ni kina nani?”

“Pale jirani na nyumba ninayoishi pana kijiwe cha vijana wasio na kazi, wanakaa hadi usiku wa manane kuvuta bangi na kuzungumza. Ninashuku wanaweza kuwa wao.”

“Sasa twende nyumbani kwako nikaone jinsi wizi huo ulivyotokea halafu unionyeshe hicho kijiwe ili hao vijana waweze kukamatwa.”

“Sawa twende.”

Walikuwapo polisi wadogo ambao wangeweza kwenda na msichana huyo nyumbani kwake ili kufanya kazi hiyo lakini nikaona niende naye mimi ili nipajue anapoishi.

Gari zote za polisi zilikuwa zimetoka ikabidi nikodi teksi kwa pesa zangu na kwenda na msichana huyo hadi nyumbani kwake Mikanjuni.

Tulipofika alinionyesha nyumba aliyokuwa anaishi mwanzo kabla ya hii anayoishi sasa.

Kabla ya kuingia ndani alinionyesha ukuta ambao wezi hao waliuruka na kuingia ndani. Tukaingia ndani ambako alinionyesha mlango wa nyuma uliokuwa umevunjwa akaniingiza katika kila chumba ambako wizi ulitokea ikiwemo chumbani kwake.

Kwa kweli wezi hao walikuwa wamemtia hasara. Wakati ananieleza machozi yalikuwa yakimtoka Hamisa. Aliniambia alitumia karibu miaka miwili kununua vitu hivyo kwa kutumia mshahara wake.

“Hivi sasa gharama zimepanda sitaweza tena kuvinunua labda kwa miaka kumi,” akaniambia.

“Usijali utanunua tu Mungu mkubwa,” nikamwambia kumpa moyo.

Hamisa akabetua mabega yake.

“Sidhani. Labda itokee miujiza”

“Kwani unaishi na nani?” nikamuuliza.

“Ninaishi peke yangu”

“Hujaolewa bado?”

“Sijaolewa.”

“Okey, sawa. Sasa twende ukanionyeshe hicho kijiwe cha hao vijana.”

Tukatoka tena. Tulipanda teksi iliyokuwa inatusubiri. Tukazunguka mtaa wa pili ambako Hamisa alinionyesha kijiwe hicho tukiwa kwenye teksi.

Kilikuwa kipo kwenye ukingo wa mfereji wa maji ya mvua uliokuwa pembeni mwa barabara.

“Vijana wanakaa pale usiku kucha, wanavuta bangi na kupiga kelele,” akaniambia.

Wakati huo hatukukuta vijana wowote.

“Wanaanza kuonekana saa kumi na moja jioni na ikifika usiku ndio linakuwa kundi kubwa. Wakati huu wa mchana wanakwepa jua.”

“Sawa. Tutawashughulikia na kama ndio waliokuvunjia watatuambia.”

Nikamrudisha Hamisa nyumbani kwake na kumuahidi kuwa usiku wa siku ile polisi watakwenda kukifuta kijiwe kile.

“Nitashukuru kaka. Ngoja nilipie pesa ya teksi.”

“Nitalipa mimi.”

Hamisa akashangaa. Badala ya mimi kutaka anipe pesa ya kunisumbua kama ilivyo kawaida ya polisi wachache walio wazembe, mimi ndio nitoe pesa yangu kwa gharama ya teksi ambayo alitakiwa alipe yeye?

Hamisa alinitulizia macho kwa sekunde kadhaa kama vile alikuwa hajawahi kuona polisi wa aina yangu.

Macho yake yakanikumbusha kitu.

“Hebu nipatie namba yako.”

Msichana akanipatia namba ya simu yake nikaiandika kwenye simu yangu na kuweka jina lake.

“Sawa, tunakwenda.”

“Asante kaka, tutaonana.”

Teksi ikaondoka. Usiku wa siku ile nilitumia cheo changu kuandaa kikosi kazi cha polisi. Nilifanikiwa kupata magari mawili ya polisi kwa ajili ya kwenda nayo Mikanjuni.

Tukaondoka saa mbili usiku kuelekea mahali hapo. Tulipofika kweli tulikuta kundi la vijana. Wengine walikuwa wakivuta bangi wengine wakila mirungi. Tuliwaona kabla ya kuwafikia, tukazima taa za mbele za gari.

Tulipowafikia karibu, polisi waliruka kwenye magari wakiwa na bunduki na kuwazunguka ghafla vijana hao.

“Mnafanya nini hapa?” nikawauliza.

“Tumekaa tu tunapunga upepo,” kijana mmoja akajibu kwa kubabaika.

“Hizo sigara mnazovuta ni sigara gani?”

Hapo sikupata jibu. Nikawaagiza polisi kuwakamata mmoja mmoja na kuwapakia kwenye magari.

Vijana hao wakaanza kusombwa na kupakiwa. Walipakiwa kwenye magari yote mawili. Hakukuwa na kijana hata mmoja aliyewahi kukimbia.

Tukawapeleka kituo cha polisi cha Chumbageni na kuanza kuwahoji mmoja mmoja. Miongoni mwa vijana hao kulikuwa na wanafunzi wa shule za sekondari, vijana wasio na kazi na wapiga debe kwenye vituo vya mabasi.

Wale ambao tuliwashuku kuhusika na uhalifu tuliwatenga kando na kuwahoji zaidi.

Kijana mmoja baada ya kuminywa alikiri kwamba kundi lao ndilo lililohusika kumuibia Hamisa lakini akadai yeye hakuhusika.

“Tutajie waliohusika,” nikamwambia kijana huyo ambaye aliwataja wenzake mmoja baada ya mwingine.

Jumla aliwataja vijana saba ambao wote walikuwa ni miongoni mwa vijana waliokamatwa. Tukawapata kirahisi.

Baada ya vijana hao kubanwa na polisi, walikiri kuhusika na wizi huo na wakakubali kwenda kuonyesha walikokwenda kuficha vitu walivyoviiba kwa Hamisa.

Usiku huo huo tuliondoka na kijana mmoja ambaye alitupeleka katika nyumba moja iliyokuwa Magomeni. Tulipobisha na kuingia ndani tukavikuta vitu hivyo ambavyo vilirundikwa katika chumba kimoja.

Aliyevinunua aliwaahidi kuwalipa siku ya pili yake. Alikuwa mfanyabiashara mmoja ambaye naye tulimkamata ingawa alidai kuwa aliwasaidia tu vijana hao kuweka vitu vyao.

Tulivipakia vitu hivyo na kuvipeleka kituo cha polisi. Asubuhi kulipokucha nikampigia simu Hamisa.

“Umeamkaje Hamisa?” nikamuuliza baada ya kupokea simu.

“Nikisema nimeamka salama nitadanganya, wiki hii yote nina zamu ya usiku. Muda huu ndio nimerudi nyumbani.”

“Pole sana, ndio maisha. Sasa Hamisa panda daladala au kodi bodaboda uje utambue vitu vyako.”

“Nije wapi?”

“Kituo cha polisi cha Chumbageni.”

“Ninakuja sasa hivi.”

Nikakata simu. Chini ya nusu saa Hamisa alishushwa na boda boda mbele ya kituo cha polisi.

Aliletwa ofisini kwangu nikampeleka mahali tulikohifadhi vitu tulivyovichukua Magomeni.

Hamisa alishukuru Mungu baada kuvitambua vitu vyake kimoja baada ya kingine.

Baadhi ya vitu alisema havikuwa vyake.

“Kwa hiyo kila kitu chako kilichoibiwa kipo hapo?” Nikamuuliza.

“Naona kama vipo vyote, lakini nitakwenda jua nyumbani,”

“Hutavichukua leo. Vitakaa hapa kama ushahidi. Kesho tunawapeleka wale vijana mahakamani.”

“Ni wale wa pale mtaani?”

“Ndiyo wale wale. Tulikwenda kuwakamata jana usiku.”

“Nakushukuru sana kwa kweli.”

“Sasa wewe nenda zako. Nitakujulisha ni lini utatakiwa kwenda kutoa ushahidi mahakamani.”

“Sawa.”

Hamisa akaondoka. Siku iliyofuata tukawapeleka mahakamani vijana wote tuliowakamata.

Vijana saba tuliwashitaki kwa uvunjaji na wizi, viijana wengine walishitakiwa kwa kosa la utumiaji wa dawa za kulevya ikiwamo mirungi na bangi. Na mfanyabiashara mmoja akashitakiwa kwa kukutwa na mali ya wizi.

Vijana wote walikana mashitaka. Kesi ikaahirishwa. Baada ya kesi kuahirishwa nikampigia simu Hamisa kumjulisha kwamba afike mahakamani siku ambayo kesi hiyo itaitishwa tena. Nilimtajia tarehe ya kesi.

Kuanzia hapo ndipo nilipoanza kuwasilina na Hamisa. Tarehe ya kesi ilipowadia Hamisa alifika mahakamani akawashuhudia vijana wake waliompaka wanja wa macho. Kesi ikaahirishwa tena. Upande wa mashitaka ukatakiwa kupeleka mashahidi.

Ndipo nikamuandaa Hamisa kwenda kutoa ushihidi wake kama mlalamikaji katika siku ambayo kesi ingeitishwa tena.

Siku ambayo Hamisa alikwenda kutoa ushahidi alikumbana na maswali ya vijana hao waliokuwa wameshitakiwa kwa kosa la wizi.

Kijana wa kwanza alimuuliza Hamisa kama alimuona wakati anavunja na kuiba nyumbani kwake.

“Sijakuona. Mimi nilikuwa kazini kwangu. Niliporudi asubuhi ndio nikakuta nimevunjiwa mlango na kuibiwa.”

Yule kijana hakutaka kuuliza swali jingine lakini swali lake hilo likaulizwa na vijana wote walioshitakiwa.

Pengine walidhani kuwa swali hilo lingesaidia kuionyesha mahakama kuwa vijana hao hawakuhusika na wizi huo kwa sababu mwenyewe hakuwaona.

Hamisa aliwaambia kuwa hakukuwa na yeyote aliyemuona kwa sababu alikuwa kazini kwake.

Baada ya Hamisa kumaliza kutoa ushihidi wake kesi ikaahirishwa tena kwa wiki mbili.

Baada ya wiki mbili hizo mimi ndiye niliyeitwa kutoa ushahidi, nikaeleza jinsi Hamisa alivyokuja kituoni na kutoa ripoti ya wizi uliofanyika nyumbani kwake.

Nikaeleza jinsi nilivyokwenda naye nyumbanni kwake na kushuhudia mlango wake wa uani ulivyovunjwa na vijana hao ambao waliruka ukuta.

Pia nikaeleza nilivyoshuhudia sebule yake ikiwa imesafishwa. Nikataja vitu ambavyo Hamisa aliniambia viliibwa nyumbani kwake wakati mwenyewe akiwa kazini.

“Nilipomuuliza mlalamikaji anashuku nani amemuibia akanitajia kundi la vijana ambalo linaweka maskani yao mtaa wa pili na ule anaoishi mlalamikaji. Usiku nikishirikiana na polisi wenzangu tulikwenda kuwakamata vijana wote tuliowakuta,” nikaileleza mahakama.

Nikaendelea kueleza kuwa katika kuwahoji vijana hao mmojawao alitueleza kuwa anawafahamu vijana waliomvunjia mlalamikaji na kumuibia.