SIMBA imerudi mazoezini ikiendelea kujipanga hapa nchini, lakini kuna kocha mmoja aliyewahi kuinoa timu hiyo ameshtuka aliposikia usajili wa mido mmoja akisema pale Msimbazi wamepata kamanda matata uwanjani.
Kocha aliyezungumza hayo ni Abdelhak Benchikha, ameshtuka kusikia kiungo Alassane Kante amesajiliwa na timu hiyo kisha akakumbuka fasta ilikuwa afanye kazi na Msenegali huyo akiwa Misri.
Benchikha ambaye aliifundisha Simba kwa miezi michache, alisema wakati akiwa Modern Future ya Misri aliwahi kukutana na jina la huyo Kante akitakiwa kusajiliwa na Waarabu hao.
Kocha huyo alisema hata hivyo, Future ilizidiwa akili na kiungo huyo kutimkia Tunisia na wakati anapitia rekodi zake aligundua alipoteza kiungo anayejua kazi uwanjani.
“Ndiyo unaniambia yule Kante yuko Simba, nakuapia kwa Mungu ni mchezaji mzuri sana wamepata. Ni kiungo ambaye ataongeza kitu kikubwa kwenye eneo la kati hasa akicheza mbele ya mabeki wa kati,” alisema Benchikha.
“Wakati tunamsajili Babacar Sarr (Simba), tulikuwa tunataka mtu kama Kante, lakini sasa amepatikana nadhani utakubaliana na maneno yangu akianza kucheza Simba.”
Akizungumzia ubora wake, Benchikha alisema Kante mbali na kujua kukaba kwa nguvu pia anajua kusogeza timu juu kwa kupiga pasi za maana, lakini kama akipata nafasi anaweza kufunga.
“Wakati nikitafuta taarifa zake niliongea na kocha mmoja anayefundisha Tunisia akaniambia namna kiungo huyo anavyocheza mtaona namna anavyojua kuleta ugumu eneo la kati. Anajua kupiga pasi na hata kusogeza timu juu, anajua pia kufunga ni mchezaji anayecheza kwa hesabu kubwa uwanjani nadhani Simba imepata kamanda mzuri uwanjani,” alisema kocha huyo.
Hata hivyo, Benchikha aliongeza, endapo Kante atakutana na kiungo mzuri wa kucheza naye sambamba, basi Simba inaweza kuwa tishio ikitegemea kama itakuwa na washambuliaji wazuri.
“Sijajua pale kati wana wachezaji gani wengine wazuri, lakini kama atakutana na viungo wazuri nadhani Simba itakuwa na kiwango bora. Najua pia kulikuwa na shida ya washambuliaji wazuri kama nao watakuwa wamepatikana itakuwa nzuri sana kwao,” alisisitiza.
Benchikha aliifundisha Simba msimu wa 2023–2024 akitokea USM Alger, ambapo aliondoka uliofuata na kutua JS Kabylie kabla ya msimu huu kurejea tena USM Alger.