Bocco alamba shavu jeshini | Mwanaspoti

NAHODHA wa zamani wa Simba na Taifa Stars, John Bocco aliyekuwa akikipiga JKT Tanzania katika Ligi ya msimu uliopita, amedaiwa kulamba shavu jipya kwa maafande hao, licha ya kwamba hatakuwa na kikosi hicho katika Ligi Kuu msimu wa 2025-26.

Bocco aliyejijengea heshima akiwa na Azam FC aliyoipandisha Ligi Kuu mwaka 2007 na kutwaa nayo mataji kadhaa ikiwamo la Ligi Kuu 2013-2014 ilikuwa ikielezwa ni mmoja ya wachezaji watakaotemwa kwa kikosi cha msimu ujao cha JKT Tanzania, lakini jamaa bado yupo jeshini.

Mwanaspoti limepenyezewa taarifa za ndani kwamba mshambuliaji mrefu mwenye umri wa miaka 36 kwa sasa amebadilishiwa majukumu JKT Tanzania, kutoka kucheza uwanjani hadi kuwa kocha wa kikosi cha timu ya vijana cha U-20.

Taarifa hizo zinasema kuwa kwa msimu ujao unaotarajiwa kuzinduliwa Septemba 16 kwa mechi ya Ngao ya Jamii kati ya watetezi Yanga na Simba, Bocco hatacheza tena akiwa na JKT badala yake atakuwa anakifundisha kikosi cha U-20 cha maafande hao wa Jeshi la Kujenga Taifa.

“Bocco alikuwa anacheza na kusomea ukocha, kutokana na kile ambacho amekifanya katika Ligi Kuu ya Tanzania, amekuwa kivutio kwa vijana wengi, ndio maana tumeamua kumpa majukumu ya kuibua na kutengeneza vipaji,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Ukitaja wachezaji wenye heshima kubwa wazawa Tanzania, jina lake ni kati ya hayo, nidhamu yake, bidii na kuipenda kazi tunaamini tutawapata kina Bocco wengine wengi katika nafasi tofauti kwenye timu yetu ya JKT Tanzania.

“Mbali na hilo Bocco ni mchezaji anayependa kazi yake na ana misimamo, hilo tunaamini litatusaidia kuwapata vijana wazuri ambao watapanda kuichezea timu kubwa.”

Kabla ya kunyakuliwa na JKT msimu uliopita baada ya kumaliza mkataba na Simba, Bocco aliwahi pia kuinoa timu ya vijana ya Msimbazi ya U17, ndipo ghafla akaibukia kwa maafande hao ambao aliwafungia mabao mawili klatika Ligi Kuu, ambapo timu hiyo ilimaliza nafasi ya sita.

Bocco ndiye mchezaji anayeshikilia rekodi ya kufunga kwa misimu 17 mfululizo ya Ligi Kuu, na pia akiwa mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu akiwa na mabao 156, akiivunja rekodi ya nyota wa zamani wa kimataifa aliyewahi kuwika Bandari Mtwara, Yanga, Simba na Taifa Stars, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyefunga mabao 153 kupitia misimu 13.

Bocco pia amewahi kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu kwa misimu miwili tofauti 2011/12 akifunga mabao 19 enzi akiitumikia Azam kabla ya kurudia 2020-21 akiwa Simba alipomaliza na mabao 16 na kuipa timu hiyo taji la mwisho katika Ligi Kuu Bara baada ya kubeba awali misimu nne mfululizo.