CCM Geita yazindua kampeni zake, mshikamano ukisisitizwa

Geita. Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Geita,  Jumanne Septemba 2, 2025 kimezindua kampeni za kuinadi Ilani ya CCM 2025-2030 kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kampeni hizo zinazinduliwa wakati majimbo saba kati ya tisa na kata 92 kati ya 122 mkoani humo, wagombea wao wanasubiri kupigiwa kura za Ndiyo na Hapana.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika katika Kata ya Uyovu Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Nicholaus Kasendamila amesema chama chao kinaingia kwenye kampeni kikiwa na mtaji mkubwa wa uadilifu, uaminifu, uchapakazi na busara ya mgombea wao wa urais, Samia Suluhu Hassan.

Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Nicholaus Kasendamila akimkabidhi Naibu Waziri mkuu Dotto Biteko ilani ya chama kwa niaba ya wagombea ubunge wenzake  kuelekea uchaguzu mkuu ujao.

Amesema kupitia kwa Samia, CCM inazo sababu za kuomba ridhaa ya wananchi kuendelea kuongoza nchi akisema Serikali aliyokuwa anayoiongoza imefanya maendeleo makubwa.

Amesema miongoni mwa mambo yaliyofanywa ni pamoja na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni lango kubwa la biashara kwaTanzania na nchi jirani.

Amesema Serikali imejenga daraja refu la Busisi, na kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere (MW 2,115) na reli ya kisasa ambayo inaendelea kufanya kazi.

Kasendamila amesema katika Mkoa wa Geita, Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025 imetekelezwa kwa mafanikio makubwa.

“Tayari tumejenga shule mpya za msingi 151, shule za sekondari mpya 118, hospitali mbili za rufaa, hospitali za wilaya mpya nne na vituo vya afya 17,” amesema mwenyekiti huyo.

Kasendamla amesema wamejenga pia zahanati 69, leseni za madini 7,600 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo na kuhusu umeme, kabla ya kuingia kwa Serikali ya awamu ya sita kulikuwa na vijiji 362 tu vyenye umeme lakini sasa vijiji vyote 486 mkoani Geita vina umeme.

Akizungumzia kuhusu miundombinu ya barabara, amesema barabara za lami na changarawe zimeendelea kujengwa mkoani Geita ili kurahisisha usafiri wa wananchi.

Ametaja vipaumbele vya CCM katika ilani ni pamoja na kuongeza fursa za wananchi kujiimarisha kiuchumi, kuendeleza sekta za afya, elimu, madini na umeme.

Mwenyekiti huyo wa CCM, amewaomba wananchi waipigie kura CCM iwaletee maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya wagombea nafasi ya ubunge mkoani Geita, Dk Doto Biteko mgombea wa Jimbo la Bukombe anayesubiri kupigiwa kura za ndiyo na hapana, amewashukuru wananchi  kwa kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi wa kampeni hizo akisema ni ishara ya wananchi kukipenda Chama cha Mapinduzi.

Amesema uchaguzi wa mwaka huu utapeleka salaam ndani ya nchi na kimataifa kuhusu uwepo wa demokrasia nchini, hivyo amewaasa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura akiahidi kuwa maendeleo zaidi yanakuja.

Amesema Mkoa wa Geita unazidi kukua na sasa ni miongoni mwa mikoa mitano yenye uchumi mkubwa kwa kuwa namba moja kwa kuzalisha dhahabu.

“Umekuwa mkoa kiungo kwa maeneo mengine nchini na watu wake ni wachapakazi hivyo  watampigia kura Dk Samia Suluhu Hassan ili kupata maendeleo zaidi,” amesema mgombea huyo.

Kuelekea uchaguzi Mkuu 2025, Dk Biteko amesisitiza uchaguzi huo uwaunganishe wananchi badala ya kuwatenganishe.

Amesisitiza kuwe na kampeni za kistaarabu na CCM kitaendelea kufanya kazi kwa umoja.

“Uchaguzi huu ni kwa ajili ya maendeleo yetu, tunataka barabara bora, umeme, afya, mitaji ya biashara, tusiuchukulie  poa uchaguzi huu kwani una maana kubwa kwenye maisha yetu,” amesisitiza Dk Biteko.

Awali, Katibu wa CCM Mkoa wa Geita, Alexandarina Katabi amesema Mkoa wa Geita una mtaji wa wapiga kura waliojiandikisha takriban 1,532,408 huku Wanaccm waliojiandikisha wakiwa ni 524,000 ikiwa ni mtaji wa nusu ya wananchi waliojiandikisha.