CCM na mkakati wa kutibu majeraha kura za maoni

Dar es Salaam. Katikati ya vinyongo vya baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kutokana na kuenguliwa katika michakato ya uteuzi wa kuwania nafasi mbalimbali, chama hicho kimeanza mkakati wa kutibu majeraha.

Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Stephen Wasira, ndiye aliyekabidhiwa kibarua hicho, akifanya ziara katika mikoa mbalimbali, hasa maeneo ambayo kumeibuka manung’uniko ya wanachama baada ya uamuzi wa vikao vya kitaifa.

Tayari juhudi hizo, zimezaa matunda kwa kufanikisha kumrejesha kundini Flatey Massay, ambaye baada ya kuenguliwa katika michakato ya ndani ya chama hicho, alihamia ACT Wazalendo na kuchukua fomu ya kuwania ubunge kwa tiketi ya chama hicho cha upinzani.

Wasira ameshafanya ziara hiyo mkoani Arusha na sasa yupo Manyara, ambapo alifanikiwa kumrejesha kundini Massay. Huku pia kuna tetesi kwamba ziara yake itafanyika kwa siku 60 za kampeni, na Kanda ya Ziwa itakuwa eneo lingine atakalotembelea.

Agosti 31, 2025, akizungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali za CCM majimbo ya Arusha Mjini, Arumeru Magharibi na Mashariki, Monduli wa Arusha, Wasira aliwataka wanachama kuacha makundi na uelekeo uwe kwenye uchaguzi mkuu.

Wasira alisema makundi yanayotokana na kura za maoni ndani ya chama hicho yamekuwa yakisababisha mgawanyiko, huku wapinzani wakipita katikati ya mgawanyiko huo.

“Kwa hiyo, kama ulikuwa na mgombea lakini hakufanikiwa, bado wewe ni mwanachama wa CCM, huwezi kupoteza lengo kwa sababu kura ya maoni imeenda kama ilivyopangwa,” alisema Wasira.

Chama hicho tawala, kupitia michakato yake ya ndani, kimeengua majina ya wabunge 133 waliohudumu katika Bunge la 12 kupitia CCM, sawa na asilimia 52.16.

Hatua hiyo ilisababisha hasira za wafuasi hao ambao baadhi walijitokeza hadharani kupinga mchakato, huku wengine wakiandamana hadi ofisi za wilaya za CCM kushinikiza kurudishwa kwa waliowaunga mkono kuteuliwa kuanzia udiwani hadi ubunge.

Miongoni mwa maeneo yaliyokumbwa na kashikashi ni pamoja na majimbo ya Tarime Mjini (Mara), Tanga Mjini na Maswa Mashariki (Simiyu) na Nachingwea.

Hata hivyo, Agosti 26, 2025, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, aliwasisitizia wanachama wa chama hicho kuheshimu uamuzi wa vikao kuhusu wagombea walioteuliwa kuwania ubunge na udiwani.

Alisema kila mwanachama wa CCM anapaswa kutambua kuheshimu chama hicho, badala ya watu ndani ya chama, akitumia msemo wa ‘chama kwanza, mtu baadaye’.

Taarifa zilizopo zinadai kuwa Wasira atakwenda katika mikoa mbalimbali, ikiwemo ya Kanda ya Ziwa, ili kutuliza hali ya hewa na kutibu majeraha ya uchaguzi wa ndani katika majimbo ambayo kulikuwa na sintofahamu.

Akizungumzia hali hiyo, Mchambuzi wa siasa, Dk Faraja Kristomus, amesema wagombea waliowekwa kando licha ya kuongoza kwa kura nyingi katika mchakato wa kura za maoni, wana wafuasi wao na wajumbe waliowapigia kura mtaji.

“Inawezekana wale wajumbe waliompigia kura mgombea wao ambaye hajapitishwa, wakafanya uamuzi wa kumuunga mkono mgombea wa upinzani atakayeshindana na yule ambaye hawakumtaka,” amesema Dk Kristomus.

Amesema Arusha, Tanga, Manyara na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa kuna changamoto ya baadhi ya watiania wa CCM walioshinda kura za maoni za chama hicho, kuwekwa kando na kuchukuliwa wengine.

“Ziara hii ya Wasira inawezekana ni njia mojawapo ya kutuliza maumivu ya uchaguzi wa ndani, hasa kura za maoni katika hayo maeneo na kuweka mikakati mipya.

“Hapo baadaye Wasira akikamilisha ziara hii, tutapata picha halisi kuhusu suala hili, kwa kuangalia maeneo atakayotembelea, ambapo tutahusianisha na ule mchakato wa kura za maoni,” ameeleza mchambuzi huyo.

Dk Kristomus amesema kuna baadhi ya maeneo wanachama wa CCM waliamua kuondoka katika chama hicho na kuhamia vyama vya upinzani, hivyo huenda ziara hiyo ikawashawishi kurejea chama tawala ili kupunguza nguvu za upinzani.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Onesmo Kyauke, amesema makundi na vinyongo ni matokeo ya kawaida ndani ya CCM kila wakati wa michakato ya uchaguzi.

Vinyongo na makundi hayo, Dk Kyauke ameeleza mara nyingi yanajitokeza pale inaposhuhudiwa aliyeongoza katika kura za maoni hakuteuliwa.

“Wakati mwingine, amesema hali hiyo inajitokeza pale inapotokea aliyekuwa mbunge kwa tiketi ya chama husika, anaenguliwa na vikao vya chama hicho kwenye michakato,” amesema.

Kwa sababu mara nyingi watu hao huwa na wafuasi, amesema ndipo makundi yanapoanza, kwa watu kuandamana, wengine kususa na wapo wanaonuna.

Dk Kyauke amesema vinyongo hivyo vimekuwa vikisababisha baadhi ya wanasiasa hao kuihama CCM na kwenda upinzani, kama ilivyowahi kushuhudiwa kwa Waziri Mkuu mstaafu, hayati Edward Lowassa, mwaka 2015.

“Hata kama mtu asipoenda upinzani, anaweza akaamua kununa tu na asisaidie kufanya kampeni. Ni jambo la kawaida na limeanza zamani ndani ya CCM,” amesema.

Kuhusu anachokifanya Wasira, amesema nacho si kipya na kitakuwa na matokeo chanya kwa chama hicho, kama ambavyo tayari kuna mwanachama mmoja (Flatey) amesharudi.

Amefafanua kuwa kinachofanywa na kiongozi huyo wa CCM ni kuendelea kutibu majeraha yaliyosababishwa wakati wa michakato ya ndani ya chama hicho, kama mkakati wa kuhakikisha kunakuwa na umoja.

Katika mazungumzo yake, msomi huyo amerejea uchaguzi wa ndani wa Chadema, akisema kilishindwa kutibu majeraha, ukizingatia kampeni zilikuwa za uhasama, ndiyo maana kumeibuka mgawanyiko wa hali ya juu.

“Kinachofanywa na Wasira kitakuwa na matokeo, na kwa sasa hakuna changamoto kubwa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, kama umeona kuna mwanasiasa alihama na sasa amerudi,” amesema.

Dk Kyauke amesema muhimu ni kuhakikisha wakati wa kampeni hakujengwi uhasama unaomvunja moyo mwingine.