Chaumma yazidi kuchanja mbuga yaingia Kilimanjaro

Kilimanjaro. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, ameendelea na kampeni zake baada ya kuhitimisha ziara ya siku tatu mkoani Tanga na apiga hodi Kilimanjaro, akilenga kuwashawishi wapigakura milioni 37.6 waliojiandikisha kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Katika uchaguzi huo unaosimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), vyama 17 vya siasa vinachuana kuwania nafasi ya Urais wa Tanzania, Ubunge na Udiwani huku kura zikiwa zimegeuka ‘soko huru la kisiasa, kila chama kinahaha kupata ridhaa ya kuongoza nchi.

Akiwa Tanga, Mwalimu alivuta maelfu ya wananchi katika mikutano ya hadhara aliyofanya Muheza, Mkinga, Tanga Mjini, Korogwe, na Mombo akinadi ajenda ya mageuzi ya kweli na kuhimiza Watanzania kufanya uamuzi mgumu ili kukwepa “ahadi hewa za kisiasa” zinazotolewa na chama tawala.

Katika hotuba zake amekuwa akiwasilisha sera mbalimbali zinazolenga kuboresha maisha ya Watanzania, ikiwemo kuboresha huduma za afya na elimu, kuongeza fursa za ajira kwa vijana, pamoja na kupambana na rushwa kwa nguvu mpya.

“Chaumma kiko tayari kuleta mabadiliko ya kweli, iwapo tutapewa ridhaa ya kuongoza, tutaongoza kwa misingi ya uwazi, usawa na maendeleo jumuishi.” amesema Salum.
Mgombea huyo anayejitanabaisha kama kiongozi wa masela amewataka wananchi kuwa makini katika kufanya uamuzi wao wa kisiasa, akikisisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi wenye maono, maadili, na walioweka mbele maslahi ya taifa.
Katika ujengaji hoja zake anaonekana kuibuka kama sauti mbadala kwa vijana na wananchi wanaotafuta mabadiliko ya kweli.

Kwa kutoa mifano na ahadi za msingi kuhusu utajiri, kuboresha sekta ya kilimo, viwanda, haki za rasilimali na ustawi wa jamii.

 

Kutengeneza matajiri vijana

Mwalimu ameahidi kuwa serikali yake itaweka mkazo mkubwa katika kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia sera madhubuti zisizo na upendeleo wala propaganda.

Akizungumza katika kata za Maramba na Mapatano, amesema:
“Sitaki vijana waendelee kubabaika. Nataka niwazalishe matajiri. Dhahabu zipo kila mahali lakini wenyeji hawaoni faida yake. Sisi tukiingia Ikulu, tutaanza kwa kufanya mageuzi ya sheria na sera za biashara ndogondogo, kuhakikisha vijana wanalindwa, wanapewa mitaji na kufuatiliwa hadi wafanikiwe,”.

Pia amekosoa Serikali ya sasa kwa kushindwa kutatua matatizo ya msingi kama barabara na maji safi, akidai kuwa hali hiyo ni mbinu ya kisiasa ya kuwaweka wananchi katika umasikini ili waendelee kutawaliwa.

“Mama mjamzito anabeba mizigo kama anaenda kuanza kidato cha kwanza Ghalanosia. Hii haikubaliki,” amesema

Mwalimu pia ameahidi kusimamia kwa ufanisi mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vijana na wanawake, akisisitiza kuwa mikopo hiyo isiendelee kuwa “mtego wa kisiasa” bali chombo halisi cha maendeleo.

 

Viwanda, kushuka bei ya petroli na dizeli

Mwalimu ameweka bayana mkakati wake wa kufufua viwanda nchini, akieleza kuwa Tanga na Morogoro zitakuwa kitovu cha mapinduzi ya viwanda Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

“Nitarejesha heshima ya kihistoria ya mikoa hii. Tanga ilikuwa kitovu cha viwanda, leo imegeuka kuwa ghala. Hili haliwezi kuendelea,” amesema.

Ameahidi pia kujenga viwanda vya kusindika matunda, kusafisha mafuta, na kufufua viwanda vya mkonge ambavyo vilikuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Mkoa wa Tanga.

“Kiwanda cha kusafisha mafuta kitajengwa Tanga kwa ajili ya kusindika mafuta yanayosafirishwa kutoka Uganda. Baada ya kiwanda hicho kujengwa, mafuta ya dizeli na petroli yatashuka na kuuzwa chini ya Sh1,500 kwa lita,” amesema.

Amesema pamoja na Tanga kuwa na reli, bandari, ardhi yenye rutuba na mkonge bado watu wake ni maskini, hali aliyosema inaashiria uzembe wa kiuongozi, hivyo Serikali ya Chaumma haitakubali.

Ahadi ya nchi ya maziwa na asali

Akiwa Muheza, Mwalimu alijikita zaidi katika ajenda ya ustawi wa taifa, akiahidi kuigeuza Tanzania kuwa “nchi ya maziwa na asali”, ambapo rasilimali zitawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi wala urasimu.

“Msiniangalie kwa umri wangu, au umbile langu, nipimeni kwa dhamira yangu na uadilifu wangu. Kama uongozi ni suala la umri, basi miaka 60 tumekabidhi nchi kwa wazee wa CCM, lakini bado hamna maji Muheza.”

Mwalimu amesema matatizo ya Watanzania hayawezi kuendelea kufichwa nyuma ya maelezo ya kisiasa au kisingizio cha bahati mbaya.

“Shida mlizonazo si za kuomba msamaha kwa Mungu, zinasababishwa na kuikumbatia CCM. Achaneni na Wazee, nichagueni Mwalimu,” amehimiza.

Aahidi pensheni ya kila mwezi kwa Wazee

Akiwa Korogwe Vijijini, hajasahau Wazee, ameahidi kuanzisha mpango wa pensheni ya kila mwezi kwa wazee wote nchini iwapo atachaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi ujao.

Amesema kuwa wazee ni nguzo muhimu ya jamii na taifa haliwezi kusonga mbele bila kutambua mchango wao.
“Tutahakikisha kila mzee anapata mafao ya pensheni kila mwezi, bila kujali kama alikuwa mfanyakazi wa serikali au la,” amesema.
Amesema aahadi hiyo ni sehemu ya sera za kijamii ya Chaumma inayolenga kupunguza pengo la kiuchumi na kuongeza ustawi wa wananchi waliotumikia taifa kwa muda mrefu.

 

Hakuna wazo la biashara la kijana litakalokufa

Katika kutambua vijana kama nguvu kazi ya Taifa, Mwalimu amewaahidi vijana akichaguliwa na kuingia madarakani hakuna wazo la biashara la kijana litakalokufa bali Serikali yake itawawezesha kwa kuwapa mitaji.

Akizungumza wakati akiwasalimia Wananchi wa Muheza akiwa njiani kutokea Tanga Vijini kwenda Korogwe Vijini, Mwalimu amesema hali ilivyo sasa kwakwe inamuumiza vijana hawaungwi mkono kwa kupewa mitaji kuwawezesha kuwa wafanyabiashara wakati na baadaye wakubwa.

“Nina waahidi nazungumza na vijana wa Kerege kwaniaba ya Vijana wa Tanzania nzima, hakuna wazo la kijana mwenzangu la kibiashara litakalokufa, wewe buni wazo au anzisha jukumu la kulinda nitalifanya nikiingia madarakani nitalinda biashara zenu zishamiri na kukua,” amesema.
Amesema katika Serikali yake hatokubali kijana kufanya kazi hadi miaka 10 bila kuendelea huku akisema labda atake mwenyewe.

Salma Soud ambaye ni mkazi wa Muheza amesema Tanzania inahitaji kupata viongozi wanaoumizwa na kero zinozosumbua jamii wakatatue.

“Wananchi wengi hatuna muono wa kujua yupi mtu sahihi labda pengine elimu ya uraia bado hatujapata, lakini kusema kweli tunahitaji mtu mwenye utashi wa kufanya mageuzi ya kweli,” amesema

Kuhusu Mwalimu, Salma amesema anajitahidi kugusia changamoto zinazowakabili Watanzania lakini wananchi watafanya uamuzi sahihi yupi wanataka awaongize.

Kwa upande wake Allen Komba Mkazi wa Tanga Mjini, amesema mkoa huo bado unatatizo kubwa la kiuchumi na ajira kwa watu wake wanahitaji mtu atakayeenda kuonyesha njia.