Dart yaomba radhi kuchelewa mwendokasi Mbagala, kuanza Septemba 15

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart), Dk Athumani Kihamia, katika mahojiano na kituo cha runinga cha Clouds ameomba radhi wananachi kwa ucheleweshaji huo, huku ikieleza sababu ya kuchelewa ni kuhakikisha vitu vyote vinavyohitaji kabla ya mradi kuanza viwe vimekamilika kwa ufasaha.

Amesema kuhusu maandalizi ya kuelekea kuanza kutoa huduma kwa mabasi hayo barabara ya Mbagala yanaendelea vizuri na huduma hiyo itaanza kutolewa ifikapo Septemba 15, 2025.

Wakati mradi wa mabasi yaendayo haraka awamu ya pili unaohusisha barabara ya Mbagala ukitarajiwa kuwa na mabasi zaidi ya 755, mgawanyo wake wa utoaji huduma  utawahusu pia wakazi wa Buza na Kigamboni.

Wakati mabasi 500 kazi yake yatakuwa ni kuwatoa abiria kutoka maeneo ya pembezoni ikuhusisha Temeke, Chamazi, Buza na viunga vyake, lakini mengine yatawabeba abiria kutoka Toangoma, Kigamboni, Vikindu na kisha kuwaleta katika kituo kikuu cha Mbagala. Hapo wataunganisha safari zao kwenda maeneo mbalimbali katikati ya jiji. Kwa Kigamboni barabara watakayoitumia ni ile inayotarajiwa kujengwa  hadi Vikindu.

Awali, huduma hizo zilikuwa zianze Septemba 1, 2025 lakini imeshindikana kutokana na kutokamilika kwa kituo cha kujazia gesi na kufungwa mageti janja yatakatumika kuchanjia kadi wakati wa kuingia kwenye vituo hivyo lengo likiwa ni kuondokana na matumizi ya tiketi hali ambayo pia itasaidia uhifadhi wa mazingira na kudhibiti upotevu wa mapato.