Datius ajipa tumaini Mtibwa | Mwanaspoti

BAADA ya kupewa miaka miwili na Mtibwa Sugar, beki wa kulia Datius Peter amesema klabu hiyo itafufua matumaini mapya kwake ya kuendeleza kipaji alichonacho kwa kucheza soka la ushindani.

Peter alijiunga na Mtibwa katika dirisha la usajili kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Kagera Sugar aliyodumu nayo tangu mwaka 2022, ambapo ameiacha baada ya kushuka daraja msimu uliopita.

Licha ya kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara na kushindwa kutoa ushindani msimu uliopita, Peter anaamini msimu huu ni wake ambapo Mtibwa itanufaika zaidi na uwezo alionao aliowahi kuuonyesha akiwa na Mbao FC, Polisi Tanzania na Kagera Sugar.

Beki huyo wa kupanda na kushuka msimu uliopita ni miongoni mwa wachezaji wachache katika Ligi Kuu Bara waliomfunga kipa wa Simba, Moussa Camara katika mchezo ambao Simba ilipata ushindi wa mabao 5-2 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu usajili ndani ya Mtibwa, Peter alisema anategemea kufanya mambo mazuri na kulipa deni la imani alilopewa na uongozi wa klabu hiyo ambayo imepanda daraja msimu huu.

“Nina furaha kuwa nimepata sehemu mpya ambayo nimeaminiwa, ninachowaambia mashabiki wa klabu yangu mpya watarajie mambo mazuri kutoka kwangu,” alisema Peter na kuongeza; “Mtibwa Sugar ni sehemu tu ya kufanya kazi kwahiyo nimeamua kuja kupambana ndiyo maana nikaamua kuja hapa kwa ajili ya kazi, mimi sehemu yoyote nafanya kazi na nipo tayari kutoa nilichonacho.”