Dk Biteko awataka wananchi kutochukulia ‘poa’ uchaguzi mkuu

Geita. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amewataka wananchi kutochukulia ‘poa’ uchaguzi mkuu ujao, bali kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025, akisema ni uchaguzi muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita, Dk Biteko amewataka wananchi kufanya uamuzi sahihi na kuwataka wagombea kufanya kampeni za kistarabu.

Amesema uchaguzi wa mwaka huu utapelekea salamu ndani na nje ya nchi juu ya demokrasia  na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa ajili ya maendeleo.

Dk Biteko ambaye ni mgombea pekee wa Jimbo la Bukombe, amesema katika miaka mitano iliyopita, Serikali imefanya maendeleo makubwa ikiwemo ujenzi wa shule za msingi na sekondari, upatikanaji wa umeme vijijini, miradi ya maji na ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Akizungumzia maendeleo ya Jimbo la Bukombe, amesema Serikali imeongeza shule za msingi kutoka 80 hadi 104 na sekondari kutoka 16 hadi 25. Kwa mkoa mzima, shule mpya 151 za msingi na 188 za sekondari zimejengwa.

Aidha, upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka asilimia 42 hadi 62 na vijiji vyote vya Bukombe tayari vimeunganishwa na umeme. Jitihada zinaendelea kufikisha huduma hiyo hadi kila kitongoji.

Mgombea huyo ametaja pia miradi inayotekelezwa ikiwamo ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa jua cha KV5 wilayani Bukombe, barabara ya Ushirombo–Katoro, na Chuo cha Veta kitakachowezesha vijana kupata ujuzi wa aina mbalimbali.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila amesema vijiji 486 vimefikiwa na umeme na sasa jitihada zinafanywa kuhakikisha kila kitongoji kinafikiwa na umeme.

Katika sekta ya afya, miradi sita imekamilika ikiwemo ujenzi wa wa hospitali mbili za rufaa ikiwemo ya Kanda Chato na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, ujenzi wa hospitali za wilaya nne, vituo vya afya 17 na zahanati 67.

Akizungumzia sekta ya madini amesema zaidi ya leseni 7,600 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo.

Katika uzinduzi huo wagombea tisa wa ubunge na 122 wa madiwani wametumia fursa hiyo kuomba wananchi kuwachagua katika uchaguzi mkuu unaaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.