Dk Kweka: Matatizo ya afya ya akili hudhoofisha utendaji kazini

Arusha. Maofisa mipangomiji wameguswa na mada ya athari za matatizo ya afya ya akili, hususan namna yanavyoweza kuathiri fikra, hisia na tabia ya mtu sehemu ya kazi.

Mada hiyo iliwasilishwa katika kikao kazi cha maofisa mipangomiji wa mikoa, kilichoandaliwa na Idara ya Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa siku tatu kuanzia Septemba 1.

Katika mkutano huo, ilibainishwa kuwa changamoto za afya ya akili zinavyoathiri uwezo wa mtu kufanya maamuzi sahihi, kushirikiana na wengine kazini, pamoja na kuhimili shinikizo la kazi.

Mada hiyo iliyotolewa na daktari bingwa wa magonjwa ya figo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Garvin Kweka, ilibainisha kwamba matatizo ya afya ya akili yamekuwa yakiongezeka kwa kasi sehemu za kazi.

Dk Kweka amesema hali hiyo hudhoofisha utendaji wa wataalamu wengi, ikiwemo kushindwa kutimiza majukumu ya kila siku kwa ufanisi.

Amesema tatizo hilo huathiri kwa kiasi kikubwa fikra, hisia na mwenendo wa mtu, hali inayoweza kusababisha mtu kupoteza ari ya kazi, kujitenga na jamii, kukosa usingizi, kuingia kwenye huzuni ya kudumu, wasiwasi kupita kiasi na wakati mwingine hata kufikia hatua ya kutaka kujiua.

Akizungumzia kuhusu akili hisia, Dk Kweka alisema ni uwezo wa mtu kutambua, kuelewa, kudhibiti na kutumia hisia zake pamoja na za wengine kwa njia chanya.

Amesisitiza kuwa akili hisia ni kipengele muhimu katika kuimarisha ustawi binafsi, hasa katika mazingira yenye changamoto nyingi kama vile kazini, nyumbani au ndani ya jamii.

“Uwezo wa mtu kuelewa na kudhibiti hisia huongeza ustahimilivu wa kiakili na kimwili. Watu wenye kiwango cha juu cha akili, hisia huwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na mfadhaiko, migogoro ya kijamii na changamoto za maisha kwa utulivu na busara,” alisema.

Oktoba mwaka jana, Serikali kupitia Wizara ya Afya ilitoa kauli ya kuhakikisha mahali pa kazi panakuwa salama na panazalisha tija kwa kushirikiana na wizara za kisekta.

Kauli hiyo ilitolewa Oktoba 10, 2024 na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dk Ahmad Makuwani, aliyemwakilisha Waziri wa Afya, Jenista Mhagama katika maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani yaliyofanyika kitaifa Dodoma.

“Tunahitaji waajiri na waajiriwa waweke mipango ya kupunguza visababishi vya magonjwa ya akili, kuhakikisha utambuzi wa mapema na matibabu, na kufanya mahala pa kazi kuwa salama na pasipo na vichocheo vinavyoweza kuathiri afya ya akili ya wafanyakazi,” alisema.

Alitoa wito kwa jamii na wadau kushirikiana na Serikali kufanikisha lengo la kuimarisha afya ya akili kazini na kwenye jamii kwa ustawi endelevu wa taifa na mtu mmoja mmoja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Tiba, Dk Hamad Nyembea, alisema huduma za afya ya akili zimeanza kupanuliwa kupitia mikakati madhubuti ya Serikali, ikiwemo kufikisha huduma hizo ngazi ya Halmashauri ifikapo 2030.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dk Paul Lawala, alisema kufuatia kaulimbiu ya maadhimisho ya afya ya akili, ni jukumu la viongozi wa rasilimali watu kulinda afya ya akili ya wafanyakazi, kutambua changamoto na kuzitatua kwa njia chanya badala ya kuwatenga, kuwaadhibu au kuwanyanyapaa.