Dodoma. Serikali imeagiza elimu ya afya kwa Watanzania ianze kutolewa katika ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu ili watu wajue namna bora ya mfumo wa kimaisha.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Septemba 3, 2025 na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ambaye amesema elimu itasaidia kuwafanya watu wajue namna ya ulaji na vyakula vinavyofaa ikiwemo kufanya mazoezi pia.
Elimu inayosisitizwa kutolewa kwa umma, ni kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, ili kuwawezesha wananchi kuepuka magonjwa hayo na gharama za matibabu.
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Kituo cha Mafunzo ya Saratani na Kituo cha Kupandikiza Figo katika hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.
Amesema maeneo mengine watu wanapata changamoto kwa sababu ya kukosa elimu, lakini akasisitiza kuwa huduma bora lazima ziambatane na nidhamu ya kitaaluma na heshima kwa wagonjwa.
“Wataalam waangalie suala la utoaji wa elimu ya afya, ni muhimu sana wakaanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu ili watu wafahamu jinsi ya kula milo inayofaa lakini wazingatie namna ya kufanya mazoezi kwa ajili ya afya zao,” amesema Dk Mpango.
Amesisitiza watumishi wa afya kutoa huduma kulingana na viwango vya vituo vyao na wafanye kazi kwa kufuata viapo vya kazi ili kuwasaidia wananchi waofika kupata huduma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Profesa Abeli Makubi amesema kwa sasa Hospitali ya Benjamin Mkapa inatoa huduma za kibingwa 20 ikiwemo ya upandikizaji uume.
Profesa Makubi ametaja huduma zingine ni kupandikiza uroto, figo, uzibuaji wa moyo na matibabu ya homoni.
Kuhusu ujenzi wa kituo cha matibabu ya saratani amesema Serikali ya Tanzania inafanya kwa kushirikiana na Japan ambapo zaidi ya Sh28 bilioni zitatumika kabla ya kufunga vifaa vyenye thamani ya Sh13.4 bilioni.
Amesema miradi hiyo inatarajia kuongeza wigo wa huduma za kibingwa na kuifanya hospitali kuwa kituo cha rejea kitaifa na kikanda kwani kituo cha upandikizaji figo kinatarajiwa kuhudumia takribani watu 14 milioni ambapo watapunguza rufaa za nje na kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa hospitali hiyo, Profesa Edward Hosea ameiomba Serikali kuongeza nyumba za watumishi na magari katika hospitali hiyo.
Profesa Hosea pia ameomba Serikali kuitangaza Benjamin Mkapa kuwa Hospitali ya Taifa, kwani inawezekana kutokana na namna inavyotoa huduma