Dk Nchimbi amkaribisha Mpina akisubiri kesi yake leo

Kisesa. Wakati shauri kupinga kuenguliwa kwa Luhaga Mpina kwenye kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, likipangwa kutajwa leo, jina lake limeibuka kwenye kampeni zinazoendelea.

Dk Emmanuel Nchimbi, mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Mapinduzi, amemtumia ujumbe Mpina akimwomba ampigie kura na arejee kwenye chama hicho tawala.

Dk Nchimbi alitoa ujumbe huo jana Septemba 2, 2025 katika eneo la nyumbani kwa Mpina – Mwandoya, Jimbo la Kisesa, mkoani Simiyu, aliposimama kuwasalimia wananchi na kuwaomba kura katika mwendelezo wa kampeni zake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2015.

Mpina ambaye ameongoza jimbo hilo kwa miaka 20, katika mbio za mwaka huu alijitosa tena lakini jina lake halikurejeshwa na Kamati Kuu ya CCM ili kupigiwa kura za maoni Agosti 4, 2025.

Kutokurejeshwa kwa jina hilo, kulimfanya waziri huyo wa zamani wa Mifugo na Uvuvi kutafuta jukwaa jingine la siasa na Agosti 5, 2025 alijiunga na ACT-Wazalendo, ambako Agosti 6, 2025 mkutano mkuu maalumu wa chama hicho ulimchagua kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, mbio zake mpya zilikutana na kikwazo baada ya Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kumwengua kwenye orodha ya wagombea wanaopaswa kuteuliwa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.

Hatua ya Uamuzi wa INEC iliegemea uamuzi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa Mpina hapaswi kuteuliwa kwa kuwa aliteuliwa na chama isivyo halali, kufuatia pingamizi la kada wa chama hicho kwamba hakuwa ametimiza mwezi mmoja ndani ya chama kama kanuni zinavyotaka.

Kufuatia sintofahamu hiyo, Mpina alifungua kesi ya kikatiba kupinga hatua hiyo na wakati kesi hiyo inaendelea leo, jana Nchimbi akamkaribisha ‘arudi nyumbani na ampigie kura’.

Mpina alipotafutwa na Mwananchi kuhusu ombi la Dk Nchimbi, alieleza kushangazwa na kauli hiyo.

“Sasa nampigiaje yeye, na mimi ni mgombea?” alihoji Mpina.

Kuhusu suala la kurejea CCM alisema: “Narejeaje CCM wakati mimi ni mgombea? Nafikiri umenielewa…”

Agosti 27, 2025 katika Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma, Bodi ya Wadhamini ya ACT-Wazalendo na Mpina walifungua shauri dhidi ya INEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uteuzi wa Mpina kuomba kuteuliwa na INEC kuwa mgombea urais wa ACT-Wazalendo, na INEC kumzuia kurejesha fomu ya kuomba uteuzi aliyokabidhiwa awali na Tume.

Katika shauri hilo namba 21692 la mwaka 2025 lililofunguliwa chini ya hati ya dharura, waombaji pamoja na mambo mengine waliiomba Mahakama iielekeze INEC ipokee fomu ya mgombea huyo kwa ajili ya uhakiki na uteuzi.

Shauri hilo linalosikilizwa na majaji Abdi Kagomba (kiongozi wa jopo), Evaristo Longopa na John Kahyoza lilitajwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 28.

Waombaji waliwakilishwa na jopo la mawakili John Seka, Edson Kilatu, John Madeleka, Mwanaisha Mdeme na Jaspar Sabuni, huku wajibu maombi wakiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method akishirikiana na Stanley Kalokola na Erigh Rumisha.

Mbali na nafuu zinazoombwa, pia Mpina aliiomba Mahakama iiamuru INEC isimamishe kwa muda mchakato wa uteuzi wa wagombea wa urais kusubiri shauri hilo kusikilizwa likishirikisha pande zote.

Mahakama katika amri zilizotolewa na Jaji Kagomba, ilikataa maombi ya kusimamisha mchakato wa uteuzi wa wagombea urais.

Hata hivyo, Jaji Kagomba alisema Mahakama ina wajibu wa kuangalia yote yaliyofanyika kama yamezingatia sheria na Katiba na kwamba, ikijiridhisha kuwa taratibu za kisheria na kikatiba hazikufuatwa katika kuondolewa kwake, haitasita kutoa amri zitakazomrudishia haki zake.

Wajibu maombi walipewa siku tano wawe wamewasilisha majibu na kiapo kinzani na shauri litatajwa leo Septemba 3.

Jana Septemba 2, Dk Nchimbi na msafara wake akitokea Itilima kwenda Meatu, alisimama Mwandoya kusalimia wananchi akawaomba Oktoba 29, 2025 waichague CCM akisema imejipanga kuendeleza miradi mbalimbali ya afya, elimu, barabara na maji.

Katikati ya kuomba kura, Dk Nchimbi akasema: “Mdogo wangu (Mpina) asiponipigia kura atakuwa amekosa adabu. Si nilikuja hapa akasema mimi ni kaka yake, basi anipigie kura.”

Dk Nchimbi akiwa katibu mkuu wa CCM alifanya ziara mkoani Simiyu na kufika eneo hilo la Mwandoya na Mpina akiwa mbunge kipindi hicho aliwaeleza wananchi wa hapo kuwa Dk Nchimbi kwake ni kaka yake na wameshirikiana tangu Umoja wa Vijana (UVCCM).

Huku wananchi wakimsikiliza jana kwenye mkutano huo, Dk Nchimbi alieleza kuwa jambo la pili kwa mdogo wake Mpina, wamfikishie salamu kuwa: “Kaka yako (Dk Nchimbi) alipita hapa, akirudi (CCM) tena nitapokea kadi yake (ya ACT-Wazalendo) na mimi nitaipokea mwenyewe kadi yake. Tunajua ukitoka halafu… unarudi.”

Miongoni mwa wana-CCM waliowahi kutoka na wakarudi ni waliowahi kuwa mawaziri wakuu, Edward Lowasaa na Fredrick Sumaye na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe. (Membe na Lowasaa kwa sasa ni marehemu).

Mkazi wa Mwandoya, Petro Njiluku, akizungumza na Mwananchi kwenye mkutano wa Dk Nchimbi, alisema: “Mpina hawezi kumpigia (kura), yaani Mpina ampigie Samia? Kwa sababu yaliyotokea sijui, ila sidhani.”

Njiluku alisema: “Hapa hawana chuki na CCM bali wana chuki kwa sababu mtu aliyeenguliwa wanampenda.”

Katika mkutano huo, Dk Nchimbi alimwita Mchungaji Peter Msigwa, kada wa chama hicho aliyewahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini (2010-2020) kupitia Chadema, kuwasalimia wananchi.

Mchungaji Msigwa alisema kazi kubwa imefanyika ya kuwaletea wananchi maendeleo.

“Na Mpina tulikuwa naye bungeni. Naamini atasikia wito wa Dk Nchimbi na atarudi,” alisema.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Kisesa, Godfrey Mbuga alisema wamejipanga kufanya siasa za kistaarabu. “Tumeshavunja makundi na tuwe kitu kimoja,” alisema akieleza utekelezaji wa ilani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kuwa ndiyo turufu yao kurudi tena kwa wananchi kuwaomba ridhaa ya kuongoza.

Mpina alipitishwa na Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo, Agosti 6, 2025 kugombea urais lakini uteuzi wake umebatilishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kutokana na pingamizi la Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala.

Monalisa alidai uteuzi huo ni batili kwa kuwa Mpina hana sifa kutokana na kutokutimiza vigezo vya kikanuni, akirejea Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa chama hicho, Toleo la mwaka 2015, kanuni namba 16(4) (i-iv).

Akirejea kanuni hizo, Monalisa alibainisha kuwa kanuni ya 16(4) (i) inaeleza mgombea wa urais/viongozi wa chama katika ngazi ya Taifa, anapaswa awe mwanachama wa ACT-Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya wagombea wa chama.

Kanuni ya 16(4)(iv) anapaswa awe ni mtu aliyethibitika kuielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za ACT-Wazalendo na aonyeshe utayari wa kuisimamia na kuiishi.

Monalisa alibainisha kuwa Mpina anakosa sifa zote hizo, kwa kuwa alijiunga na chama hicho Agosti 5, 2025 na alipitishwa na mkutano mkuu kuwa mgombea wa chama hicho Agosti 6, siku moja baada ya kujiunga na chama hicho.

Msajili wa Vyama vya Siasa baada ya kusikiliza pande zote alikubaliana na hoja za pingamizi la Monalisa na kutengua uteuzi wa Mpina.