Maswa. Kushinda uchaguzi wowote ni mbinu na mikakati. Mgombea humpasa kuwa mbunifu ili jamii au kundi analotaka kulifikishia ujumbe ili limuchague unapaswa kujipanga vyema.
Siasa ni sanaa ya kushawishi, kupanga, kuelewana na kuongoza watu kwa ustadi na hekima. Lengo upate unachokitaka.
Hii ni kwa sababu siasa, haitegemei tu kanuni au sheria, bali pia ustadi wa binadamu kuelewana, kujadiliana na kushawishi.

Katika hilo, Dk Emmanuel Nchimbi, mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) anatumia utani wa Wangoni na Wasukuma kupenyeza sera zake.
Wasukuma na Wangoni kiasili ni watani. Dk Nchimbi ni Mgoni. Tangu ameanza kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 mikoa ya Kanda ya Ziwa amekuwa akiwaeleza;
“Ninyi Wasukuma, nimeamua kuanzia huku kwa watani zangu, sasa ole wenu msituchague.”
Dk Nchimbi alianza kampeni hizo Agosti 29, 2025 majimbo mbalimbali ya Mwanza, akaenda Mara, Simiyu na sasa yupo mkoani Shinyanga.

Leo Jumatano, Septemba 3, 2025
Akihutubia mkutano wa kampeni eneo la Lalago, Jimbo la Maswa Mashariki, mkoani Simiyu ameeleza jinsi Wasukuma walivyofanikisha safari yake ya kwanza ya kwenda Ulaya.
“Niliambiwa mkutano utakuwa mdogo tu lakini Wasukuma wengi mmejitokeza, nashukuru watani zangu mmejaa wengi. Nawashukuru sana sana,” amesema.
Dk Nchimbi amesimulia jinsi Wasukuma mwaka 1998 walivyomwezesha kusafiri kwenda Ulaya katika nchi ya Ufaransa kwa kuratibiwa na mbunge wa zamani wa Maswa, Dk Pius Ng’wandu.
Amesema Dk Ng’wandu akiwa waziri wa Sayansi na Teknolojia ambaye alikuwa rafiki wa baba yake, John Nchimbi wakifundisha shule moja mkoani Iringa amesema:
“Aliniuliza wewe Mngoni, washamba sana. Akaniuliza wewe Mngoni umefikia Ulaya, mimi nikajua ni utani wa Wasukuma.”

Amesema siku chache baadaye, wasaidizi wa Dk Ng’wandu wakamtafuta ili kuanza taratibu za safari huku yeye akiendelea kuwaza kwamba utakuwa ni utani lakini: “Wasukuma wakafanikisha mimi mgoni kwenda Ulaya.” Amesema walikwenda katika mkutano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco);
“Msukuma (Dk Ng’waru) akaniambia wewe Mngoni, sasa ili ujifunze, unapaswa kukaa karibu na Msukuma na mimi kila alipopita Msukuma, nilikuwa pembeni yake.”
Wakati akisimulia hayo, wananchi na wafuasi wa CCM walikuwa wakiangua vicheko.
Dk Ng’wandu anayemwelezea, alifariki dunia Desemba 19, 2020 katika Hospitali ya Bariadi, mkoani Simiyu, baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Akizungumzia ufugaji, mgombea mwenza huyo amesema ukishughulika na mifugo; “Wasukuma wanakuwa hawana shida kabisa, sisi Wangoni ni mahindi. Lakini ukiwa na mahindi huwezi kula peke yake, utahitaji nyama na hapo ndipo ndugu zangu Wasukuma wanahitajika.”
Akiomba kura, Dk Nchimbi amesema; “Watani zangu kwa heshima zote za Wangoni, namna pekee ya kumwonesha mgombea wetu wa urais, Mama Samia (Suluhu Hassan) anapata kura nyingi, wabunge na madiwani ni kujitokeza kupiga kura. Kwa hiyo watani zangu Wasukuma msiniangushe tarehe 29 Oktoba.”
“Sasa msipojitokeza kumpigia kura, tutawapeleka Ungonini,” amesema Dk Nchimbi ambaye mara kadhaa kwenye mikutano yake amekuwa akitumia utani huo na kueleza ndio maana ameamua kuanzia mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mgombea mwenza huyo amesema, miongoni mwa ahadi ambazo Rais Samia amezitoa atakazozitekeleza ndani ya siku 100 ni kuanzishwa kwa tume ya maridhiano.
“Katika mambo ambayo Serikali ya CCM itayafanya ndani ya siku 100 ni kuanzishwa kwa Tume ya Maridhiano ili Watanzania wote wasikilizwe, amani, umoja uendelezwe.
Watanzania wote tuwe kitu kimoja. Wale wengi wasikilizwe, wale wachache wasikilizwe. Tunataka nchi iwe na watu wanaosikilizana na wanaoelewana,” amesema.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed amesema wanaendelea kufanya kampeni ili kuhakikisha wanapata ushindi wa kishindo wa kura za Rais, madiwani na madiwani.
Kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa amesema hakuna chama kinachoweza kuwaletea maendeleo wananchi zaidi ya Chama cha Mapinduzi.
Mchungaji Msigwa amesema amekuwa upinzani (Chadema) kwa zaidi ya miaka 10, mjumbe wa kamati kuu; “Hakuna kitu, Tanzania hii chini ya Mama Samia, iko mikono salama kabisa, wala msidanganyike.”
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua yanayotolea kwenye mikutano ya kampeni ya Dk Nchimbi Kanda ya Ziwa.