EQUITY NA TALEPP KUZINDUA MAPINDUZI SEKTA YA NGOZI

::::::

Benki ya Equity Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na Chama cha Watengenezaji wa Bidhaa za Ngozi Tanzania, TALEPPA, kwa lengo la kufungua fursa mpya katika sekta ya ngozi na kuimarisha viwanda vya ndani,Makubaliano hayo yameambatana na uzinduzi wa Mradi wa Viatu vya Shule Tanzania, TALSSI, unaolenga kuongeza thamani ya ngozi ya ndani na kuchochea ajira.

Akizungumza katika tukio hilo lililofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara Wizara ya Viwanda na Biashara, Sempeho Manongi, ameipongeza Benki ya Equity kwa kusaidia wafanyabiashara wa ndani kupata mikopo, akisema sekta ya ngozi kwa muda mrefu imepuuzwa kwa kudhaniwa haikopesheki.

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Kilimo Biashara kutoka Benki ya Equity, Teofora Madilu, amesema benki hiyo imejipanga kutoa mikopo mahsusi kwa wafugaji, wauzaji wa ngozi mbichi na viwanda vidogo ili kuhakikisha thamani ya mifugo inanufaisha pia wafugaji kupitia ngozi bora na bidhaa zenye ushindani.

Katibu wa TALEPPA, Timoth Funto, amesema chama hicho kimepanga kuzalisha jozi milioni 10 za viatu vya shule kila mwaka vyenye thamani ya shilingi bilioni 300, hatua inayotarajiwa kutoa ajira kwa zaidi ya watu milioni mbili na kupunguza uagizaji wa viatu kutoka nje unaokadiriwa kufikia jozi milioni 54 kila mwaka.