Folz ana jambo lake Yanga

YANGA wameliamsha wakianza rasmi leo safari kuelekea kilele cha Wiki ya Mwananchi, lakini kule kambini Kocha Romain Folz akipunguza dozi kidogo huku mastaa wa timu hiyo wakipelekwa kambi moja ya jeshi.

Takriban wiki mbili nyuma kule kambini, Yanga ilikuwa ni mwendo wa dozi kali za mazoezi yakifanyika mara mbili kwa siku – kama sio kuanzia gym, basi timu ilipaswa kuwa ufukweni kisha jioni uwanjani.

Huko uwanjani ilikuwa kuchezea mpira kidogo tu, lakini nafasi kubwa ilionekabana sawa na mazoezi ya asubuhi kwa mastaa wa timu hiyo kuongezewa pumzi na stamina.

Kuanzia wiki hii Folz amepunguza dozi na sasa kikosi hicho kinajifua mara moja kwa siku na kama siyo asubuhi, basi jioni pekee.

Ratiba hiyo mpya imekuwa ikitawaliwa na mbinu zaidi za uwanjani, ambapo kinapigwa sana kule Avic huku mastaa wa timu hiyo wakiendelea kuzibeba falsafa za kocha wao huyo raia wa Ufaransa.

Yanga imeendelea kucheza mechi za kirafiki ambazo Folz anazitumia kupima mazoezi wanayofanya na baada ya kuipiga Tabora United 4-0 Ijumaa iliyopita, kesho watacheza mchezo mwingine.

Folz ameomba mchezo wa kirafiki mgumu wa ugenini, na akapewa JKT Tanzania ambao kwa miaka misimu miwili  hawajawahi kuwafunga wanajeshi hao wakiwa nyumbani.

Yanga itajipima na JKT katika uwanja wa maafande hao wa Meja Jenerali Isamuhyo, ambapo Folz amewapeleka mastaa wake wote waliosalia kambini wakiwemo Pacome Zouzoua na Mamadou Doumbia.

Wakati wiki ijayo Yanga na Simba watakuwa na matamasha yao ambapo Simba itaanza Septemba 10 na Simba Day, upande wake Yanga itakanya hivyo Septemba 12 katika kilele cha Wiki ya Wananchi.

Siku chache zilizopita Simba ilizindua tamasha lake Mafinga mkoani Iringa, lakini Yanga wanazindua Wiki ya Mwananchi leo kwenye Viwanja vya Zakhem, Mbagala, Dar es Salaam.

Yanga jana ilitambulisha kaulimbiu ya tamasha hilo ambalo litakwenda na ‘Tunapiga kichwani’ ikilenga kuendeleza vipigo zaidi kwa wapinzani.

Meneja wa Habari wa Yanga Ally Kamwe alisema leo wanazindua hamasa ambapo watatambulisha ratiba kamili ya wasanii watakaoipamba siku hiyo Septemba 12 pale Uwanja wa Benjamin Mkapa.