BAADA ya kuambulia pointi moja kupitia suluhu ya mechi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Kagame 2025, kocha Miguel Gamondi amesema walikosa mchezaji mbunifu wa kufungua ukuta wa wapinzani wao, Coffee ya Ethiopia huku akimtaja Marouf Tchakei.
Singida ilipata suluhu ya mechi za Kundi A ya michuano hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, jijiji Dar es Salaam dhidi ya Wahabeshi hao ambao Gamondi alikiri walifanikiwa kuwadhibiti kutokana na kuingia na mbinu ya kujilinda zaidi, huku Singida ikikosa mbinu za kupenya ukuta huo ili kupata matokeo mazuri zaidi.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Gamondi alisema Singida ilicheza vizuri kwa kutawala mchezo, lakini ilishindwa kupata ushindi kutokana na ugumu wa wapinzani wao ambao walijilinda zaidi kwa dakika zote 90.
“Nakiri kuwa tulikosa ubunifu hatukuwa na mchezaji ambaye angeweza kufungua ukuta wa Coffee tumecheza bila Khalid Aucho, Tchakei ambaye ni mbunifu katika eneo la umaliziaji tulikuwa na mshambuliaji mpya Mishamo Daudi na Andrew Phiri ambao pia ni wapya kikosini,” alisema Gamondi na kuongeza;
“Wachezaji hao hawajafanya mazoezi na sisi kwa muda wana mbili hadi tatu tangu wameungana na sisi hii haiwezi kuwa sababu kubwa ni kuhakikisha tunaterngeneza ubora kwenye eneo la ushambuliaji kuanzia mita 25 ili kuwa na safu nzuri.”
Gamondi alisema bado hawafahamu wachezaji wake vizuri lakini anaamini anakikosi kizuri licha ya mapungufu yaliyoonekana eneo la ulinzi wapo vuzuri shida ni kumalizia.
“Ni kwa mara ya kwanza wamecheza mechi ya ushindani kwa dakika 90 wachezaji wangu wameonyesha udhaifu mkubwa kwenye kufunga eneo la ulinzi ndio lilionyesha ubora zaidi hivyo nina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha wachezaji wangu wanapata muunganiko mzuri na kuwa na umakini kwenye umaliziaji.”
Singida inayoshiriki michuano hiyo kwa msimu wa pili mfululizo, itashuka uwanjani kesho dhidi ya vinara wa Kundi A, Polisi Kenya walioifumua Garde Cotes ya Djibouti kwa mabao 4-0.