KOCHA wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi ametangaza kuwa lengo kubwa kwenye michuano ya Cecafa Kagame Cup 2025 ni kuipa timu yake ubingwa akiitumia pia kama sehemu ya maandalizi ya mashindano ya kimataifa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Gamondi, aliyewahi kuinoa Yanga, ameanza jana, Jumanne safari yake na Singida kwenye mchezo wa Kundi A kwa kucheza dhidi ya Ethiopian Coffee kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo baada ya pambano la ufunguzi kati ya Kenya Police na Garde Cotes ya Djibouti.
Kocha huyo, alisema mashindano hayo ni daraja la kujenga kikosi imara kitakachoshindana ndani na nje ya nchi.
“Nataka kuona timu yangu ikicheza kwa ushindani mkubwa na kupigania ubingwa. Kagame Cup ni kipimo kizuri kwa maandalizi ya Kombe la Shirikisho la CAF na msimu mpya wa ligi,” alisema Gamondi.
Singida Black Stars watakuwa na nyota wapya akiwemo kiungo mshambuliaji wa Zambia, Clatous Chota Chama, aliyesajiliwa akitokea Yanga pamoja na kiungo mkabaji wa Uganda Cranes, Khalid Aucho, atakayejiunga na timu baada ya majukumu ya timu ya taifa.
Hii ni mara ya kwanza kwa Singida BS kushiriki michuano hiyo ambayo fainali itachezwa Septemba 15 kwenye uwanja wa KMC.
Mashindano ya Cecafa Kagame Cup 2025, yanashirikisha jumla ya timu 12 huku Rais wa Rwanda, Paul Kagame, akiendelea kuunga mkono michuano hiyo ya ukanda wa Afrika Mashariki na kati.