Jalada kesi ya bosi wa Jatu, linapitiwa na kusomwa upya

Dar es Salaam. Serikali imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa jalada la kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi Mkuu  wa Kampuni ya Jatu  PLC, Peter Gasaya (33), linapitiwa na kusomwa na timu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka( NPS), makao makuu Dodoma.

Baada ya kupitiwa na kusomwa upya kwa jalada hilo, timu hiyo italitolea uamuzi na uamuzi huo utawasilishwa katika Mahakaka hiyo.

Hayo yameelezwa leo Septemba 3, 2025 mahakamani hapo na wakili wa Serikali, Roida Mwakamele, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Gusaya anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea” amedai wakili na kuongeza.

“Pia jalada la kesi hii, bado linaendelea kusomwa na timu kutoka Dodoma, hivyo kwa sababu hiyo upande wa mashtaka tunaomba mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi wa kesi hii umekamilika au laa,” amedai Mwakamele.

Mwakamele baada ya kutoa taarifa, mshtakiwa Gasaya alinyoosha mkono juu akiashiria kuwa anaomba mahakama impe nafasi ya kuzungumza na alipopewa nafasi hiyo, aliomba Mahakama hiyo isimamie kesi hiyo ili upelelezi wa shauri uweze kukamilika kwa haraka.

Mshtakiwa huyo pia aliomba mahakama ipange tarehe ya karibu ili kujua majibu ya jalada hilo baada ya kusomwa na timu hiyo ya waendesha mashtaka kutoka Dodoma.

Hakimu Mhini alisema kesi hiyo ni ya uhujumu uchumi na mahakama yake haina uwezo wa kufanya chochote isipokuwa kama itapewa kibali na DPP.

Hakimu Mhini baada ya kueleza hayo, alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 10, 2025 itakapotajwa.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili, halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa, kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5,139,865,733 kutoka Saccos ya Jatu.

Mshtakiwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya Jatu kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa sio kweli.

Shtaka la pili ni kutakatisha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam.