Dar es Salaam. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Makini, Coaster Kibonde, amesema wakipata ridhaa ya wananchi na kuingia Ikulu, watasimamia vipaumbele vitatu vya elimu, kilimo na afya.
Kibonde ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho amesema ametembea mikoa 10 katika kusaka wadhamini na amebaini vipaumbele hivyo vitatu Watanzania wamevikubali na hawatakuwa na sababu ya kutowapigia kura.
Amesema hayo leo Jumanne Septemba 2, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho uliofanyika viwanja vya Bakhresa, vilivyoko Manzese, wilayani Ubungo, Dar es Salaam.
Katika elimu, Kibonde amesema kuanzia ya awali itakuwa bure, hivyo amewaomba Watanzania wawaunge mkono ili kwenda kutimiza malengo yao.
“Makini tunaamini ukimnyima kijana elimu ni sawa na umekwenda kumfunga kifungo cha maisha na ieleweke kuwa, hatuendi tu kutoa elimu, bali elimu bora,” amesema.
Kuhusu elimu ya juu, amesema watampatia kila kijana elimu ya chuo kikuu kwa gharama yoyote inayopatikana duniani na hakutakuwa na kurudisha mikopo ya elimu.

Katika afya, amesema endapo wananchi watawaamini na kuwapa ridhaa watajenga hospitali kila kata na kila moja itakuwa na vifaatiba na siyo majengo tu.
Kwa upande wa kilimo amesema Chama cha Makini kinakwenda kumkomboa Mtanzania kumwezesha kuondokana na jembe la mikono.
“Serikali ya Makini inakwenda kufanya mapinduzi ya viwanda ambavyo pamoja na mambo mengine, vitakwenda kuzalisha mali zinazohusiana na kilimo, ikiwamo pembejeo. Mkulima hatakweda kusubiri pembejeo bali pembejeo ndizo zitamsubiri mkulima,” amesema.
Wakati huohuo, amesema wakiingia madarakani mtu wa kwanza kumuajiri atakuwa Samia Hassan Suluhu.
Amesema atampa ajira Samia, ambaye ni mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwa ni mbobezi katika masuala matatu.
Ameyataja maeneo ya ubobezi wa Samia ambaye ni Rais anayemaliza muda wake kuwa ni katika masuala ya diplomasia kwa ujumla, diplomasia ya uchumi na ya siasa.
“Hivyo mama Samia atakwenda kufanya kazi kwenye madawati matatu ya kidiplomasia niliyoyasema hapo. Watu wengine wote mtanisubiria hadi hapo tutakapobadilisha mfumo wa Katiba,” amesema na kuongeza:
“Hii ni kwa kuwa tumeamini wagombea wote wana nia njema ya kujenga nchi yao kwa masilahi mapana ya Taifa.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, ambaye ni mgombea urais wa Zanzibar, Ameir Hassan Ameir, ameasema wakichaguliwa kushika dola, watawapatia vijana kuanzia miaka 21 hadi 35 ekari tano za ardhi bure.
Amesema wanafanya hivyo kwa kuwa kwa muda mrefu vijana hawaaminiwi katika taasisi za fedha wanapohitaji mikopo.
Ameir amesema kwa kuwa viwanja hivyo vitakuwa na hati, vitawasaidia kwani vitatumika kama dhamana ya kuomba mikopo na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Makamu mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Grace Ngonyani amewaomba wananchi kukichagua Chama cha Makini kwa kuwa sera zake ni makini kama kinavyoitwa.
“Hivyo, ikifika Oktoba mumpatie mgombea Kibonde kura za ndiyo kwani ni kijana mwenye nguvu zake, mzalendo mwenye mikakati na malengo ya kweli,” amesema Grace ambaye pia ni mgombea ubunge Jimbo la Ubungo kupitia chama hicho.
Mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Azza Haji Suleiman, amewataka vijana kuepuka kuvuruga amani, akiwataka wakumbuke wana wazazi na ndugu, hivyo ikivurugika hawatakuwa na pa kukaa.