Kipagwile ajishtukia Dodoma Jiji | Mwanaspoti

MFUNGAJI namba mbili katika kikosi cha Dodoma Jiji kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita 2024-2025, Idd Kipagwile, amesema anajiona ana deni kubwa ndani ya kikosi hicho.

Kipagwile anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara, alifunga mabao saba na asiti nne akizidiwa bao moja na Paul Peter aliyekuwa kinara wa ufungaji kikosini hapo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kipagwile amesema haikuwa rahisi kwake kufikisha mabao hayo, lakini ushirikiano alioupata kutoka kwa wenzake kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi, vilimrahisishia kazi hiyo.

Kipagwile ameongeza, kutokana na hilo, anaona ana deni kubwa msimu wa 2025-2026 kuhakikisha anaendeleza ubora huo kwa lengo la kufanikisha malengo ya timu na ya kwake binafsi.

“Sio rahisi kwa ligi yetu kufikisha mabao saba hata kama yamefungwa kwa njia tofauti, lakini najivunia hilo na ninahisi nina deni kubwa sana kuelekea msimu huu.

“Nadhani mashabiki wangu binafsi na wapenzi wa Dodoma wanatamani kuona naendelea kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita, kwa hiyo nina kazi kubwa ya kufanya.”