Dar es Salaam. Safari ya kuomba ridhaa ya kuwaongoza wananchi katika uchaguzi visiwani Zanzibar haikuwahi kuisha ahadi, zikiwamo zenye vituko na mbwembwe ndani yake.
Ukiacha ile ya kuwanunulia wanahabari pikipiki za magurudumu matatu ‘bajaji’ kutoka India iliyotolewa katika uchaguzi wa mwaka 2020, sasa imeibuka nyingine ya ruhusa ya kilimo cha bangi ili kuukwamua uchumi wa Zanzibar.
Sambamba na hiyo, yupo mtiania aliyeahidi kumlipa kila Mzanzibari mshahara wa Sh500,000 kwa mwezi, iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano.
Ahadi hizo zimeambatana na nyingine ambazo aghalabu zinajirudia, ikiwamo kuboresha huduma za afya, kuwainua wanawake, fursa za ajira utatuzi wa changamoto za watumishi wa umma na kuwatetea madereva daladala na pikipiki.
Hata hivyo, wachambuzi wa siasa, wanasema ahadi hizo ndicho kipimo kitakachotumiwa na wananchi kumchagua kiongozi na mwenye nafasi zaidi ni yule aliyeahidi mambo yanayoakisi mahitaji ya jamii.
Hayo ni machache kati ya mengi, yaliyoshuhudiwa kutoka kwa watiania wa urais kutoka vyama 17, walipokwenda kuchukua fomu za uteuzi katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ulioanza Agosti 30 hadi Septemba 1, mwaka huu.
Mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, Mohamed Ibrahim Rajab amesema pamoja na ahadi kutolewa, muhimu ni kupima kwa kiasi gani zinatekelezeka.
“Nyuma ya ahadi zilizotolewa na wagombea, kuna jambo la kupima ni kwa kiasi gani zinatekelezeka na kwa kiasi gani zinaweza kuwa na kikwazo katika utekelezaji wake. Hii inatokana na wananchi wana upeo gani wa kuzisikiliza ahadi hizo,” amesema.
Amesema kuna ahadi moja kwa moja zinaakisi mahitaji ya jamii ikiwamo ya upatikanaji wa ajira, kipimo sahihi ni kuangalia kwa kiasi gani wagombea wamelitaja suala hilo.
Rajab amefafanua kuwa, kuna watu waliopo kwenye madaraka watajinadi kwa namna walivyozitekeleza, je walichokitekeleza ndicho ambacho jamii ilikuwa inakihitaji.
“Kwa mfano hivi sasa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanasema tumetekeleza au ilani imetekeleza lakini je, kilichotekelezwa ndicho kilikuwa kikihitajika katika jamii?
“CCM wamejitahidi katika ujenzi wa miundombinu ikiwamo barabara, lakini nyuma ya utekelezaji huo ni kwa kiasi gani wameisaidia jamii kwenye mambo kadhaa, moja kwa kiasi umeliendeleza suala la Umoja wa Kitaifa au umelibomoa?
Mbali na hilo, Rajab amesema baadhi ya wagombea wamekuwa wakiahidi ahadi mbalimbali, lakini hawaonyeshi namna au njia watakazozitumia katika kuzitekeleza.
“Sote tunahitaji hiki, lakini wagombea hawaonyeshi ni vipi tutafikia kwenye hicho. Bado wagombea wameshindwa kutufafanulia au kutuonyesha njia namna watakavyozitekeleza ahadi hizo,” amesema Rajab.
Miongoni mwa ahadi zilizozua gumzo ni ile ya mtiania wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya AAFP, Said Soud Said aliyesema ataanzisha kilimo cha bangi kwa ajili ya dawa na kuukwamua uchumi wa visiwa hivyo na haitatumika kuvuta.
“Zipo nchi duniani zimekuwa na madeni makubwa na zimeamua kulima bangi ili kupata fursa ya kulipa madeni hayo. Katika bara la Afrika kuna nchi zinalima bangi zingine zimejitangaza, nimeamua kuja na kipaumbele hiki ili kunyanyua maisha ya vijana,” amesema Soud.
Hata hivyo, utekelezwaji wa ahadi hiyo, unakinzana na Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kudhibiti Dawa za Kulevya kinachosema, “Hakuna mtu yeyote atakayepanda, kulea, kutengeneza au kushughulika kwa namna yoyote ile na mmea wa bangi (cannabis) au mirungi (khat), isipokuwa kwa ruhusa mahsusi iliyotolewa chini ya sheria hii.”
Hata hivyo, sheria hiyo imependekeza adhabu kwa atakayekiuka kifungu hicho ambayo ni kifungo kisichopungua miaka 20 na iwapo atakuwa amejihusisha kwa kiwango kikubwa, anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha.
Huyu ndiyo Soud ambaye kabla ya pazia la kuchukua fomu kufunguliwa alitoa ahadi ya kupiga marufuku utengezaji wa vitanda vyenye ukubwa wa futi sita kwa sita, badala yake mafundi watapaswa kutengeneza vitanda vyenye ukubwa wa futi tatu kwa nne ili kuongeza kizazi.
Soud alisema ahadi itatekelezwa endapo akifanikiwa kushinda urais wa Zanzibar, ambapo atahakikisha vijana wote wanaoa kwa fedha za Serikali na hakuna mtu atakayetoa fedha yake mfukoni kwa ajili ya shughuli hiyo.
Sambamba na hiyo, ahadi nyingine imetolewa na mtiania wa urais kupitia Chama cha Makini, Ameir Hassan Ameir amesema iwapo akipata ridhaa atatoa Sh500,000 kwa kila Mzanzibari kila mwezi kwa ajili ya kujikimu.
Amesema ahadi hiyo ataietekeleza baada ya kula kiapo cha urais bila kuchelewa, huku akisema mshahara wa kima cha chini utakuwa Sh1.5 milioni.
“Kuna watu wamekuwa na maulizo hizi fedha zitatoka wapi, lakini naomba niwatoe wasiwasi siku ya kurejesha fomu baada ya kuteuliwa na Tume nitakuja kuwaeleza chanzo cha fedha hizo zitakapotoka,” anasema Ameir.
Pia, amesema atatetea madereva wa daladala na bodaboda kwa hiyo wanaowanyanyasa wajiandae kisaikolojia kukumbana na rungu lake.
Mtiania wa nafasi hiyo kupitia ACT Wazalendo, Othman Masoud amesema dhamira yake ni kuleta mabadiliko Zanzibar, akisema wakati sahihi ni sasa.
“Dhumuni la kuchukua fomu ni kuwawezesha Wazanzibari kupata chaguo kile ambacho muda mrefu wamewekeza kunitayarisha ili nije kuwatumikia. Sasa wakati wa kuvuna ndio huu,” amesema Othman.
Kwa upande wa mtiania wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amesema analenga kuibadilisha Zanzibar ili iwe kama mataifa ya nje huku akisema chama hicho kitahubiri amani katika kampeni zake.
Dk Mwinyi anayewania urais kwa muhula wa pili, amewataka viongozi na wagombea wa CCM kuepuka siasa za chuki, ubaguzi, matusi na kuwagawa watu.
“Tuwaambie Wazanzibari tutawanyia nini, sina shaka wote watatuchagua. Sasa hivi tunakwenda na mambo makubwa mapya yatakayoibadilisha Zanzibar iwe kama nchi za wenzetu huko nje,” amesema.
Mtiania urais kupitia Chama cha UDP, Neema Salim Hamad amesema iwapo tume ikimpitisha kuwania nafasi hiyo na akapata ridhaa kutoka kwa wananchi amejipanga kuhakikisha anatetea haki za wanawake na watu wenye ulemavu.
Mbali na hilo, pia amesema vipaumbele vyake vingine ni kuimarisha huduma za afya, maji na elimu ambapo mambo hayo yote yanawagusa wanawake moja kwa moja na kuwasababishia changamoto za hapa na pale.
Amewataka wanawake kuondoa woga wakitambua kwamba wanaweza kufanya mambo makubwa na kupambania haki zao bila kujiweka nyuma.
“Iwapo nikipata urais vipaumbele vyangu ni kushughulikia mambo ya wanawake, watu wenye ulemavu, maji, elimu na afya, wanawake waondoe woga wajue kwamba tunaweza, wapambanie haki zao bila kujiweka nyuma,” amesema.
Pia, amesema kwa wafanyakazi wa umma atashughulikia changamoto zao.
Kwa upande wa mtiania urais kupitia Chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP), Hamad Mohamed Ibrahim amesema iwapo wakipata ridhaa watabadilisha kabisa mfumo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ambapo kutakuwa na serikali inayoongozwa na Rais na kurejesha mfumo wa Waziri kiongozi na naibu Waziri kiongozi.
Katika mfumo huo anaokwenda kubadilisha, mtiania huyo amesema Naibu Waziri kiongozi atatoka kwenye chama cha upinzani.
“Lakini jambo kubwa itakuwa Zanzibar ya viwanda kuzalisha ajira kwa vijana hivyo kutakuwa na vinu vya nyukilia kimoja kitakuwa Unguja na kingine Pemba na kuzalisha umeme wa kutosha ili kuwezesha viwanda hivyo kufanya kazi,” amesema Ibrahim.
Pia, vinu hivyo vya nyuklia vitasaidia kwa ajili ya ulinzi wa nchi ili kama kuna masula ya uhalifu na kuhatarisha amani ya nchi kuwe na uwezo wa kuyakabili.
“Tumejipanga vizuri sana na wananchi wanatukubali, kwa hiyo tuna imani na tume ya uchaguzi kwamba uchaguzi utakuwa wa haki na usawa na atakayeshinda atatangazwa kushika madaraka, sisi ni miongoni tunaotarajia kushika wadhifa huo,” amesema.
Amesema watabadilisha baadhi ya vifungu vya sheria lengo ni moja tu kuijenga Zanzibar.
Mtiania urais kupitia chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed amesema bado kuna mambo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi akitolea mfano wa kuagiza chakula kutoka nje ambapo takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 75 Zanzibar chakula kinaagizwa.
Kwa mujibu wa mtiania huyo, iwapo akipitishwa na tume na kupewa ridhaa ya wananchi wanakwenda kushughulikia changamoto hiyo ndani ya muda mfupi kwani kumekosa ubunifu wa kiutendaji.
Amesema ADC wameona umuhimu wa kushughulikia jambo hilo na ikizingatiwa ana uzoefu wa kushughulikia matatizo tangu alipokuwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi mwaka 1982, alipita magerezani na kubaini njaa kisha akamweleza Rais wakati huo Hayati Julius Nyerere kisha akamtaka amshauri kupata mwarobaini wa tatizo hilo na kweli ulipatikana.
Amesema mara nyingi watu wanakwenda kwa Rais wakiwa na matatizo lakini hawaendi na ufumbuzi wa matatizo.
Kwa mujibu wa Hamad, Zanzibar inahitaji hekta 10.000 kuzalisha tani 250 za mchele na uwezo huo upo ndani ya miaka mitatu chama hicho kikipata ridhaa ataweza kufanya hivyo.
Mbali na kushughulikia upatikanaji wa chakula, pia amesema atahakikisha anashusha bei ya nyama kutoka Sh15,000 ya sasa hadi Sh7,000 kwa kilo moja.
“Wavuvi wakipewa vifaa, wakulima wakapewa vifaa bure ndani ya mwaka mmoja bila kukopeshwa na kupewa mafunzo, ninaamini Wazanzibari watakula vizuri, watapata maisha mazuri,” amesema.
Amesema kuyapata hayo wanahitaji Dola za Marekani milioni 100 ambazo kuzipata ni rahisi ikizingatiwa sekta moja tu ya utalii ina uwezo wa kuzalisha.
Kama fedha zikikusanywa vizuri zikapelekwa wakulima na wavuvi Zanzibar itaondokana na shida ya chakula na hili linawezekana katika mipango mathubuti waliyonayo chama hicho. “Karafu na mwani tutaishghulikia mpaka wakulima wapate mambo mazuri,” amesema.
Mtiania kupitia chama cha DP, Shaffii Hassan Suleiman amesema jambo la kwanza wakipata madaraka ni kuhakikisha amani ya nchi inaendelea kudumishwa kwani bila hilo hakuna kinachoweza kufanyika.
Pamoja na amani, amesema watahakikisha ajira kila mzanzibari anapata kazi ya kumwingizia kipato kwani kwa sasa bado kuna changamoto kubwa na vijana wengi wanaangaika mitaani.
Kingine ambacho kinatarajiwa kufanywa na mtiania huyo baada ya kupata ridhaa ni kuongeza masoko na viwanda vingi kwa ajili ya uzalishaji na bidhaa zitakazozalishwa zipatiwe masoko nje ya nchi.
“Mimi mwenyewe ni mkulima najua changamoto zao kwa hiyo tunataka wakulima wanufaike, hata uzalishaji unaofanywa kwa sasa hakuna viwanda vya kusindika kwa hiyo kazi yetu kubwa itakuwa ni kuweka mazingira mazuri kujenga viwanda na kutafuta masoko,” amesema Shaffii.