Moshi. Mamia ya waombolezaji wamejitokeza katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Moshi Mjini, kuaga mwili wa Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini ya kanisa hilo, Dk Martin Shao (86).
Dk Shao ambaye alihudumu kama Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini kuanzia mwaka 2004 hadi 2014 alipostaafu na alifariki dunia Agosti, 25, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC iliyopo Moshi mjini mkoani Kilimanjaro.
Mwili wa Dk Shao unaagwa leo, Jumatano Septemba 3, 2025, katika Usharika wa Moshi mjini, huku mamia ya waombolezaji wakiwamo waumini wa kanisa hilo, wachungaji na wafanyabiashara, wamejitokeza.

Bada ya mwili huo kuagwa leo, utasafirishwa kupelekwa nyumbani kwake Mwika Lole na kesho Septemba 4, 2025, utazikwa katika Usharika wa Lole, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Juzi akitoa taarifa, Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk Fredrick Shoo alisema wameondokewa na kiongozi ambaye ameacha alama zisizofutika katika dayosisi hiyo na hata kwa mtu mmoja mmoja.
“Ni msiba mkubwa ambao umetugusa sisi sote, wa kuondokewa na baba yetu na kiongozi wetu, napenda kusema kwa watu wote, watoto, majirani na washarika wote wa dayosisi hii, tufarijike katika bwana na Mungu mwenyewe atutie nguvu tulipokee kama watu wa imani,” amesema.
Aliongeza kuwa; “Tumeondokewa na kiongozi ambaye ameacha alama katika Dayosisi hii, ameacha alama nyingi za kukumbukwa kwa mtu mmojammoja na kwa ujumla wake akiwa kama kiongozi wetu, kipekee katika Usharika wa Moshi Mjini tangu akiwa mchungaji katika usharika ule akiwa msaidizi wa Askofu, lakini alitangulia kuwa mkuu wa jimbo.”

Amesema “Tunafahamu unyenyekevu wake, utulivu wake na kujitoa kwake kwa ajili ya huduma hii, kibinadamu tulitamani kuendelea kuwa na baba huyu lakini tunafahamu tumewekewa mipaka, hatuna mamlaka ya kuamua mwisho wa mtu uweje.”
1966-1974 alikuwa mchungaji wa Dayosisi ya Kaskazini, 1974-1976 alikuwa Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki, 1976-2004 alikiwa msaidizi wa Askofu Dayosisi ya Kaskazini na mwaka 2004-2014 alikuwa Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini.

Askofu Dk Shao ambaye alikuwa askofu wa Tatu wa Dayosisi ya Kaskazini, alikuwa kiungo muhimu katika umoja wa kanisa, jumuiya za kanisa na taasisi za ndani na nje ya nchi.
Ametajwa kama kiongozi aliyetumikia kanisa na jamii kwa uaminifu, Askofu aliyejali mambo ya kiroho, mtetezi wa haki na usawa.