TIMU ya Coastal Union imeendelea kuboresha kikosi chake kwa ajili ya kufanya vizuri msimu unaoanza Septemba 17, ambao mechi ya ufunguzi ya Ligi Kuu itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Chanzo cha uhakika kililiambia Mwanaspoti, uongozi wa timu hiyo umemsainisha kipa Wilbol Maseke mkataba wa miaka miwili, ukiamini uzoefu wake utakuwa msaada kwa timu.
Msimu uliopita Maseke aliichezea KMC lakini hakuwa na nafasi kubwa katika kikosi cha kwanza, hivyo alimaliza akiwa na clean sheets tatu, huku akijifunga kwa msimu wa pili mfululizo.
“Vitu vikubwa vilivyotushawishi kumsainisha Maseke ana uwezo wa kuokoa mipira ya karibu ya mtu na mtu, penalti na mwepesi wa kuziona hatari kabla ya kumfikia golini kwake, kubwa zaidi anajua kuwapanga mabeki,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Maseke hadi anasajiliwa kocha alipata nafasi ya kumuona katika mechi mbalimbali za kirafiki, kwani tulikuwa naye kambini pia tumeachana na kipa Aaron Kalambo, hivyo ujio wake ni mbadala.”
Kipa huyo aliyeibuliwa na timu ya vijana ya Azam U19 kabla ya kupandishwa kikosi cha wakubwa 2021 na kuidakia timu hiyo kabla ya mwaka juzi kutua KMC kwa sasa ana umri wa miaka 25 na anatua kwa Wagosi.