Shinyanga. Jimbo la Shinyanga Mjini, ni moja kati ya majimbo ya Chama cha Mapinduzi (CCM) yaliyokuwa na mvutano mkali katika mbio za kumpata mgombea ubunge katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Kati ya watinia lukuki waliojitokeza, Patrobasi Katambi na Stephen Masele ndiyo walikuwa katika vuta nikuvute kubwa. Wawili hao, wamekuwa kwenye ‘vita’ ya kuwania kupeperusha bendera ya CCM mwaka 2020 na 2025.
Masele alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka kumi mfululizo hadi 2020 ambapo Katambi alimuangusha kwenye michakato ya ndani. Mwaka 2025 wakaingia tena kwenye mbio na mwisho Katambi akaibuka mshindi.
Masele amewahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Katambi kwa sasa ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Mvutano wa wawili hao kwenye kinyang’anyiro hicho umehitishwa leo Jumatano, Septemba 3, 2025 na mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi katika mkutano mkubwa wa kampeni za uchaguzi mkuu, uliofanyikia Uwanja wa Jasco Ngokolo, Shinyanga Mjini.
Dk Nchimbi kabla ya kuwaita jukwaani, ameanza kuelezea jinsi CCM na Serikali yake ilivyofanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya afya, kilimo, mifugo, elimu, ujenzi wa barabara na watakavyoendeleza mambo hayo kwa kasi zaidi.
Amesema hayo yametekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amewaomba wana Shinyanga kumpa kura za kutosha Oktoba 29:”Ili aendeleze alipoishia. Hakuna shaka kwamba amefanya makubwa na kila mmoja anaona.”
Dk Nchimbi amesema, Rais Samia ameahidi mambo 12 ambayo atayafanyia kazi katika siku 100 baada ya kuingia madarakani na moja wapo ni maiti zisizuiwe hospitalini.
“Rais ameahidi, kutakuwa na utaratibu ili mtu anapofariki, maiti isizuiwe, watu wapewe mpendwa wao wakamhifadhi, madeni yatalipwa,” amesema Dk Nchimbi huku wananchi wakishangilia.
Baada ya kumaliza kumwaga sera, Dk Nchimbi akawatambulisha wagombea ubunge wa majimbo mbalimbali ya mkoa wa Shinyanga. Kila mgombea aliitwa mbele na kujirambulisha jina na jimbo lake kisha wanarudi kukaa.
Walipomalizika, Dk Nchimbi akasema kuna mtu anatakiwa akamtafute popote alipo mgombea ubunge wa Shinyanga Mjini, Patrobasi Katambi ili amlete.
Huku umati wa wananchi na wana CCM wakishangilia na wasijue nani anayekwenda kupewa jukumu la kumtafuta Katambi, Dk Nchimbi akasema:”Masele kamtafute Katambi niletee hapa.”
Masele aliyekuwapo mkutanoni, alikwenda ambapo Katambi amekaa, akamchukua na kusogea naye mbele karibu na alipokuwa Dk Nchimbi akihutubia huku shangwe kutoka kwa wananchi mkutanoni hapo likisikika
Dk Nchimbi alimpa nafasi Masele kuzungumza ambapo amesema:”Mimi ndiye niliyemwachia mpira Katambi mwaka 2020 na mwaka 2025 tumeingia tena ulingoni, akanipiga dobo akasinda.”
Huku watu wakicheka na kushangilia, Masele akasema:”Sasa fainali ni tarehe 29, kombe lazima lije CCM. Naomba nimwombee kura Rais na mgombea mwenza.”
Akiendelea kuzungumza, Masele akawaomba wananchi waliokuwapo mkutanoni akisema:”Tuweke mkono moyoni, tuweke mkataba wa moyo. Hatuna cha kuwapa, CCM itashinda. Wale waliokuwa wanafikiria fikiria, timu yetu ni moja ushindi ni wa CCM.”
Amemwombea kura Katambi akisema ni:”Kizazi kipya, amefanya kazi kubwa. Yeye ndiye aliyeibuka mshindi. Hatuna sababu ya kuchanganya mafiga.Tumchague Katambi, madiwani na Rais.”
Aidha, amesema wakati Dk Nchimbi anaingia mkutanoni, alimwona akiwa ameshika simu yake mkononi:”Sasa naomba nipewe kazi ya kushika simu yake tu kila anapokwenda. Hata aniombe nani sitampa.”
Kwa upande wake, Katambi amesema kazi kubwa imefanyika ya mradi mbalimbali na kuwaomba wananchi waichague tena CCM kwa maendeleo endelevu.
Dk Nchimbi akahitimisha kwa kumtambulisha Katambi akisema:”Nawakabidhi rasmi, mgombea wa Shinyanga Mjini, Katambi, ana rekodi iliyotukuka. Amekuwa naibu waziri bora kabisa kati ya naibu mawaziri wetu.”
Amewaomba wampe kura nyingi na za mfano ili aweze kuendelea maendeleo ya Shinyanga Mjini kwa kushirikiana na madiwani na Rais Samia.
Awali, Katibu wa Oganizesheni, Issa Gavu Ussi amewaomba wananchi wasichanganye betri na kurunzi katika kuchagua viongozi watakaokwenda kutumikia wananchi.
“Siku ya kupiga kura chagueni viongozi wote kutoka Chama cha Mapinduzi, msichanganye betri na kurunzi, chagueni wabunge, madiwani na Rais wa CCM, moja ya ahadi ya Rais Samia ndani ya siku 100 za kwanza ni kuondoa ukuta na kuweka daraja la mawasiliano kati ya wananchi na serikali ili kuimarisha ushirikiano na mawasiliano bora,” amesema Gavu.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa akijibu maombi ya Gavu ameahidi kuwa wana-Shinyanga hawawezi kuchanganya kurunzi na betri akitumia lugha inayotumika kwa wanashinyanga.
“Hatuwezi kuchanganya kurunzi na betri, sisi kwa Shinyanga huwa tunasema, hatuchanganyi ng’ombe na mbuzi kwenye zizi moja, tutakwenda kupiga kura ya ndio kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi katika mkoa wetu,” amesema Mlolwa.