Dar es Salaam. Benki ya CRDB imetangaza kufunga huduma katika matawi yake yote kwa siku tatu kuanzia Septemba 5 hadi 7 mwaka huu.
Kufungwa kwa matawi hayo kunalenga kutoa nafasi kwa wataalamu kufanya maboresho na kuweka mifumo ya kisasa ili kuongeza ufanisi huduma zinazotolewa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na benki hiyo kwa umma, ndani ya kipindi husika, huduma zote za benki hazitapatikana kwa namna tofauti ambapo Ijumaa ya kuamkia Septemba 5, 2025 watu hawatakuwa na uwezo wa kupata huduma kwa saa mbili.
Pia, wateja hawatakuwa na uwezo wa kupata huduma usiku wa kuamkia Ijumaa kuanzia saa 6:00 usiku hadi saa 8:00 usiku.
Usiku wa kuamkia Jumapili ya Septemba 7, 2025, huduma zote hazitapatikana kwa saa sita kuanzia saa 6:00 usiku hadi saa 12:00 alfajiri.
Mbali na hilo, CRDB imesema huduma zitakazopatikana nje ya vipindi vya kusitishwa huduma ni ATM ambapo watu wataweza kutoa fedha na kuhamisha fedha.
Pia, malipo kupitia mashine za malipo yaani POS watu wataendelea kuzitumia kama kawaida katika utoaji wa huduma.
Huduma zingine ambazo zitaendelea kupatikana ni SimBanking watu wataweza kuhamisha fedha ndani ya mfumo wa Benki ya CRDB, kwenda mitandao ya simu, kwenda benki nyingine kupitia TIPS, kuangalia salio, kutoa fedha bila kadi kupitia ATM na malipo kwa wafanyabiashara wa TIPS/ TanQR.
“Wateja wanashauriwa kukamilisha miamala yao yote mapema kabla ya muda wa kusitisha huduma wakati ambao timu yetu ya wataalamu imejipanga kuhakikisha huduma zinarejea kwa wakati,” imesema taarifa hiyo.
Hili linafanyika wakati ambao CRDB inasherehekea miaka 30 ya uongozi na ubunifu huku ikiweka lengo la kuboresha huduma wanazotoa kwa wananchi.
Katika ujumbe wake wa kuadhimisha miaka 30 ya Benki hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Profesa Neema Mori alisema wameendelea kuimarisha mifumo ya utawala, kuendeleza mpango mkakati na kukuza utamaduni wa kufikiria mipango ya muda mrefu ujao.
Hiyo ni kuanzia kuongoza mabadiliko ya kidijitali nchini hadi kupanua huduma zao kwenda Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ujumuishi wa kifedha na maendeleo endelevu huku sera zao zikiihakikishia Benki ya CRDB kuendelea kuwa mbele ya mwelekeo wa sekta na kuendeleza misingi waliyoanzisha.
“Maono ya Bodi sio tu kuangalia miaka 30 ijayo kama mwendelezo wa yale tuliyoyafikia, ila kama lango la fursa mpya. Tunaiona Benki ya CRDB ikiwa taasisi ya fedha yenye nguvu kikanda na kimataifa. Ni benki ya kisasa, inayoongozwa kwa takwimu na ubunifu wa hali ya juu,” alisema.
Amesema katika maono yao wanaiona benki inayotumia teknolojia kama akili mnemba, ‘blockchain’ na majukwaa ya kidijitali kuhudumia wateja wake barani Afrika na duniani kote.
“Katika miaka 30 ijayo, tunalenga kukuza mizania yetu ifike kati ya Shilingi trilioni 60 hadi shilingi trilioni 70, kutoa huduma katika angalau nchi 8 duniani, kutambulika miongoni mwa benki 10 bora barani Afrika kwa ubunifu na uaminifu wa wateja na kuendeleza uongozi wetu katika usimamizi, utawala bora, na miradi endelevu,” alisema.