Maximo aanza Kagame Cup 2025, APR kicheko

KMC inayonolewa na kocha Marcio Maximo imeanza vyema michuano ya Kombe la Kagame 2025 kwa kuifumua Mlandege ya Zanzibar kwa mabao 3-2.

Ushindi huo umeifanya KMC kuwa timu ya kwanza Bara kuzoa pointi zote tatu, baada ya jana Singida Black Stars kubanwa na Coffee ya Ethiopia iliyomaliza pungufu na kutoka suluhu jana kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.

Katika mechi ya jioni ya leo  kwenye Uwanja huo, KMC ilizianza dakika 45 za kipindi cha kwanza kwa kasi  huku ikitumia mabeki wa pembeni kupandisha mashambulizi akiwemo Abdallah Lanso upande wa kulia.

Bao la kwanza kwa vijana hao wa Maximo lilitokana na kona ya dakika ya 19  huku Juma Sagwe akimalizia kwa kichwa ambacho kilimshinda kipa wa Mlandege, Hamad Ubwa na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko kifua mbele.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na KMC ikionekana kusaka bao la pili, ndipo katika dakika ya 48 ilipenyezwa krosi ya chini chini kutoka winga ya kushoto na Rashid Chambo aliyekuwa ndani ya eneo la hatari alimalizia mpira huo na kuifanya Mlandege kuwa na mlima mrefu wa kupanda.

Kazi nzuri iliyofanywa na Lanso, ilijipa mwishoni mwa kipindi cha pili katika dakika ya 86 baada ya kufunga bao la tatu kufuatia kuachia mkwaju mkali kisha kuwaomba radhi waajiri wake hao wa zamani.

Licha ya kuwa nyuma kwa mabao 3-0, Mlandege ilijaribu kurudi mchezoni na kupata mabao mawili ndani ya dakika mbili, 89 na 90 yakifungwa na Abeid kwa mkwaju wa penalti pamoja na Hafidh.

Katika mechi hiyo, Mlandege licha ya kuwa na wachezaji kutoka Ulaya na hata Amerika ya Kusini, kama vile Enzo Claude na Vitor de  Souza  ilishindwa kufua dafu na kujituka ikianza kwa kupoteza katika mashindano hayo.

Baada ya ushindi dhidi ya Mlandege, kituo kinachofuata kwa KMC ni Jumamosi kucheza mechi yao ya pili ya hatua ya makundi dhidi ya Bumamuru ya Burundi ambayo mapema mchana wa leo, ilichapwa mabao 2-0 dhidi ya APR ya Rwanda.