Pangani. Mfanyabiashara wa mkaa, Michael Yohana (43), amekutwa amefariki dunia pembezoni mwa tanuru la mkaa wakati akiendelea na shughuli za kuandaa tanuru hilo kwa ajili ya uzalishaji.
Akisimulia tukio hilo wakati wa shughuli za mazishi yaliyofanyika leo, Jumatano Septemba 3, 2025, katika Kijiji cha Langoni wilayani Pangani, mke wa marehemu, Sophia Marandu, amesema tukio hilo lilitokea jana Septemba 2, saa 11 jioni.
Sophia amesema alifika eneo la tanuru na kukuta mkaa unaungua, lakini hakuona mtu yeyote akiuchota.

Amesema hali hiyo ilimtia wasiwasi, na ndipo alipoanza kumtafuta mumewe kwa kuzunguka nyuma ya tanuru hilo.
Sophia amesema alikuta mwili wa mume wake ukiwa pembezoni mwa tanuru, tayari akiwa amefariki dunia na kuungua sehemu mbalimbali za mwili.
“Nilipofika pale tunapochoma mkaa kwenye tanuru nilikuta mkaa unateketea na mtu simuoni, ikanilazimu nizunguke nyuma ya tanuru nikamkuta amekufa, kabla sijahakikisha kwamba amefariki nilimshika kwanza na kuanza kumuita ila kila nilivyojaribu kumuamsha hakuamka amelala chali na majeraha tumboni na maeneo mengine,” amesema Sophia.
Ameongeza kuwa baada ya hapo alikimbia kwenda nyumbani huku akipiga kelele za kuomba msaada na watu walijitokeza wajue kuna tukio gani, na baada ya kuwaeleza waliongozana nae kwenda kwenye tanuru hilo kushuhudia na kuangalia jinsi ya kutoa msaada.
Sophia ameeleza kuwa watu walipofika hapo walishuhudia mwili na kubaini kuwa tayari alishafariki dunia, na kuanza taratibu za kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola kwa ajili ya taratibu nyingine za kisheria.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Langoni, Ahamad Issa amesema alipokea taarifa ya tukio hilo na kufika eneo husika, ambapo walikuta mwili huo ukiwa pembeni ya tanuru na kuonekana alishafariki tayari.
Amesema anamfahamu marehemu kama mfanyabiashara wa mkaa kijijini hapo kwa muda mrefu, hivyo baada ya kupewa taarifa aliwasiliana na polisi kata na kupewa maelekezo kuwa wananchi wasifanye jambo lolote hadi wafike.
“Tulifika eneo la tukio na kushuhudia mwili wa Michael pale chini na kuonyesha tayari alishafariki dunia, nilishirikiana na wananchi na polisi kuhakikisha taratibu zote zinakwenda sawa na mwisho tulipewa mwili na kuurudisha nyumbani kwaajili ya mipango mingine za mazishi,”amesema Mwenyekiti Ahamad.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amekiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, uchunguzi unaendelea kujua chanzo kamili cha kifo cha mfanyabiashara huyo wa mkaa, aliyefariki dunia pembeni ya tanuru lake.
Amesema ni kweli amefariki dunia akiwa pembeni ya tanuri kwenye msitu unaofahamika kwa jina la Amboni, ambapo yeye na mke wake wanajishughulisha na biashara ya mkaa na jana mkewe alimkuta amefariki akiwa kwenye shughuli hiyo na bado sababu kamili ya kifo hicho inaendelea kuchunguzwa.
“Jana majira ya saa 5 asubuhi marehemu alimuaga mkewe kwamba anakwenda kwenye tanuru lao katika msitu wa Amboni, ila majira ya saa 11 jioni mkewe alimfuata kwenye tanuru ndipo alimkuta ameanguka na alishakufa huku akiwa na majeraha katika mwili ya kuungua na moto inawezekana ilikuwa ni kwenye juhudi za kujiokoa,” amesema Kamanda Mchunguzi.
Marehemu Michael amezikwa jioni ya leo Septemba 3, 2025 kijijini kwake Langoni baada ya polisi kukabidhi mwili familia walipomaliza taratibu zao za kazi.