Mgombea urais Chaumma aahidi pensheni kwa wazee wote akiwa rais

Tanga. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi kuanzisha mpango wa pensheni ya kila mwezi kwa wazee wote nchini, iwapo atachaguliwa kuwa rais katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.

Mwalimu amesema wazee ni rasilimali muhimu kwa taifa na mchango wao haupaswi kusahaulika.

Amesema ili kutambua mchango huo, akipatiwa ridhaa na wananchi, Serikali atakayounda itakuwa rafiki kwa kundi hilo la ili lione thamani yake.

Ameeleza hayo kwa nyakati tofauti leo Jumatano, Septemba 3, 2025 kwenye mikutano yake ya kampeni iliyofanyika Korogwe Vijijini na Mombo mkoani Tanga.

Mwalimu amesema wazee ni nguzo muhimu ya jamii, taifa haliwezi kusonga mbele bila kutambua mchango wao.

 “Tutahakikisha kila mzee anapata mafao ya pensheni kila mwezi, bila kujali kama alikuwa mfanyakazi wa Serikali au la, kikubwa wazee wangu niombeeni, kazi hii si rahisi, nikiingia ikulu siwezi kuwasahau najua machungu na magumu mnayopitia,” amesisitiza.

Amesema ahadi hiyo ni sehemu ya sera za kijamii za Chaumma inayolenga kupunguza pengo la kiuchumi na kuongeza ustawi wa wananchi waliotumikia taifa kwa muda mrefu.

Mwalimu amesema Chaumma kiko tayari kuleta mabadiliko ya kweli na iwapo kitapatiwa ridhaa, kitaongoza kwa misingi ya uwazi, usawa na maendeleo jumuishi.

Mgombea huyo amewataka wananchi kuwa makini katika kufanya uamuzi wa kupiga kura akikisisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi wenye maono, maadili na walioweka mbele masilahi ya taifa.

Katika hatua nyingine, Mwalimu ameahidi kuwa Serikali yake itaweka mkazo mkubwa katika kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia sera madhubuti zisizo na upendeleo wala propaganda.

Akizungumza katika kata za Maramba na Mapatano, Mwalimu amesema: “Sitaki vijana waendelee kubabaika. Nataka niwazalishe matajiri. Dhahabu zipo kila mahali lakini wenyeji hawaoni faida yake. Sisi tukiingia ikulu, tutaanza kwa kufanya mageuzi ya sheria na sera za biashara ndogondogo kuhakikisha vijana wanalindwa, wanapewa mitaji na kufuatiliwa hadi wafanikiwe.”

Amekosoa Serikali ya sasa kwa kushindwa kutatua matatizo ya msingi kama ya barabara na maji safi, akidai kuwa hali hiyo ni mbinu ya kisiasa ya kuwaweka wananchi katika umasikini ili waendelee kutawaliwa.

“Mama mjamzito anabeba mizigo kama anaenda kuanza kidato cha kwanza shule ya sekondari, hii haikubaliki,” amesema.

Hivyo, ameahidi kusimamia kwa ufanisi mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vijana na wanawake huku akisisitiza kuwa haipaswi kuwa mtego wa kisiasa, bali chombo halisi cha maendeleo.

Viwanda, bei ya petroli na dizeli

Katika hatua nyingine, Mwalimu aliweka bayana mkakati wake wa kufufua viwanda nchini, akieleza kuwa Tanga na Morogoro zitakuwa kitovu cha mapinduzi ya viwanda Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

“Nitarejesha heshima ya kihistoria ya mikoa hii. Tanga ilikuwa kitovu cha viwanda, leo imegeuka kuwa ghala. Hili haliwezi kuendelea,” alisema.

Ameahidi Serikali ya Chaumma itajenga viwanda vya kusindika matunda, kusafisha mafuta na kufufua viwanda vya mkonge ambavyo vilikuwa uti wa mgongo wa uchumi kwa Mkoa wa Tanga.

“Kiwanda cha kusafisha mafuta kitajengwa Tanga kwa ajili ya kusindika mafuta yanayosafirishwa kutoka Uganda. Baada ya kiwanda hicho kujengwa, mafuta ya dizeli na petroli yatashuka na kuuzwa chini ya Sh1, 500 kwa lita,” amesema

Amesema pamoja na Tanga kuwa na reli, bandari, ardhi yenye rutuba na mkonge, wananchi wa mkoa huo bado ni masikini hali inayoashiria uzembe wa uongozi, hivyo Serikali ya Chaumma haitakubali hali hiyo.

Akiwa Muheza, Mwalimu alijikita katika ajenda ya ustawi wa taifa akiahidi kuigeuza Tanzania kuwa ‘nchi ya asali na maziwa’ akisema rasilimali zitawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi wala urasimu.

“Msiniangalie kwa umri wangu au umbile langu, nipimeni kwa dhamira yangu na uadilifu wangu. Kama uongozi ni suala la umri, basi miaka 60 tumekabidhi nchi kwa wazee wa CCM, lakini bado hamna maji Muheza,” amesema.

Amesema matatizo ya Watanzania hayawezi kuendelea kufichwa nyuma ya maelezo ya kisiasa au kisingizio cha bahati mbaya.

“Shida mlizonazo si za kuomba msamaha kwa Mungu, zinasababishwa na kuikumbatia CCM. Achaneni na wazee, nichagueni Mwalimu,” amewaomba wananchi waliokuwa wakimsikiliza.

Akizungumza kando ya mkutano huo, Salma Soud aliyekuwa akimsikiliza mgombea huyo amesema Tanzania inahitaji kupata viongozi wanaoumizwa na kero zinazowasumbua wananchi na kusudi azijengee mkakati wa kuzitatua.

“Wananchi wengi hatuna uwezo wa kujua yupi ni mtu sahihi, labda pengine elimu ya uraia bado hatujapata, lakini kusema kweli tunahitaji mtu mwenye utashi wa kufanya mageuzi ya kweli,” amesema Soud.

Kwa upande wake, Allen Komba Mkazi wa mjini Tanga, amesema mkoa huo bado unatatizo kubwa la kiuchumi na ajira kwa watu wake, hivyo wanamuhitaji kiongozi atakayeonyesha njia sahihi ya kutatua kero hiyo.