Tanga. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan ameshiriki kwenye msiba wa mama wa mwandishi wa habari wa Redio Mwambao FM ya jijini Tanga, Mwanamkuu Issa, huku akisema amekatisha ziara Dar es Salaam na kuamua kuhudhuria msiba, lakini ataendelea na kampeni zake za kuomba ridhaa ya wananchi katika kiti cha urais mkoani humo.
Doyo amefika msibani hapo saa 5:30 asubuhi akiwa ameambatana na Katibu wake wa NLD Mkoa Tanga, Boniface Gideon na viongozi wengine wa chama hicho.
Hata hivyo, baada ya kufika msibani hapo, baadhi ya waombolezaji walioneka kuwa na shauku ya kutaka kusalimiana naye.
Akizungumza msibani hapo, Doyo amesema alikuwa na ratiba ya kuwepo Dar ea Salaam ila imebidi kuikatisha na kuja Tanga, baada ya kupata taarifa ya msiba wa mama mzazi wa Mwanamkuu ambaye amefanya naye kazi kwa muda mrefu hasa kazi za kihabari.

“Tumekuja kumhani mwanahabari nguli ambaye nimefanya naye kazi kwa muda mrefu kwenye tasnia hii ya habari, hapa nina kofia mbili, nimekuja kama mwanahabari lakini huyu ni Mtanzania na aliyefiwa ni mwenzetu, hivyo nimeguswa, ndiyo sababu nimekuja,” amesema Doyo.
Amesema msiba ni tendo la huruma na mtu akisikia mwenzake amefiwa, anapaswa kuguswa na kwenda kushiriki mazishi na hio ni jambo ambalo haliwezi kuzoeleka kwenye jamii.
Akizungumzia ratiba ya kampeni ya chama chake, amesema inaendelea vizuri na amewashukuru wadau wanaoendelea kumpa ushirikiano kwa kuwa mpaka sasa hakuna changamoto kubwa aliyokumbana nayo ikawa kikwazo cha kuwakwamisha.

“Ratiba yetu kesho tutakuwa na mkutano wa hadhara Tanga mjini katika kunadi sera zetu kwa wananchi eneo hili, Tanga ni nyumbani kwetu na nina imani wananchi wa mkoa wangu hawataniangusha, NLD tuna uhakika wa kupata kura za kutosha,” amesema Doyo.
Doyo ni mkazi na mzaliwa wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga katika Kata ya Misima, ambapo alianza siasa akiwa cha CUF baadaye alihamia ADC na mapema mwaka huu alijiunga na NLD na kupata nafasi ya kugombea urais.