BAADA ya kushindwa kung’ara msimu uliopita akiwa na kikosi cha Mashujaa, winga Emmanuel Mtumbuka amesema ni wakati wa kufanya vizuri na kuonyesha uwezo wake baada ya kutimkia Tanzania Prisons ya Mbeya.
Mtumbuka aliyedumu Mashujaa kwa mwaka mmoja baada ya kujiunga nayo msimu uliopita akitokea Stand United ya Shinyanga, alishindwa kupata uhakika wa namba na sasa amesajiliwa na Prisons kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Akizungumza na Mwanaspoti, mchezaji huyo alisema yuko tayari kwa ajili ya ushindani ndani ya kikosi hicho ambacho kimefanya maboresho makubwa baada ya msimu uliopita kunusurika kushuka Ligi Kuu Bara.
“Maisha ya mpira ndivyo yalivyo hauwezi kukaa tu sehemu moja. Pia Prisons walikuwa wakinihitaji muda mrefu, hivyo nimeona siyo mbaya kuja huku,” alisema Mtumbuka.
Winga huyo alisema matarajio yake ni kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri na kukuza kiwango chake ili baadaye acheze soka la ngazi ya juu nchini na hata nje ya nchi.
“Binafsi napambana kuhakikisha nafanya vizuri, mambo mengine ni mipango ya Mwenyezi Mungu. Viongozi na mashabiki nawaomba ushirikiano timu iweze kutimiza malengo iliyojiwekea kwa sababu tukiwa pamoja tunaweza kuwa na msimu bora kuliko uliopita,” alisema.
Mbali na nyota huyo, maafande wa Prisons wamewasajili Michael Mtunda, Omary Mbuji, Neva Kaboma, Masoud Cabaye, Marco Mhilu na Heritier Lulihoshi.