Mwalimu mkuu, mlinzi mbaroni tuhuma za kumfanyia ukatili mwanafunzi

Arusha. Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ngarenaro, Mussa Luambano (50) na mlinzi wa shule hiyo, Olais Mollel (33), wakituhumiwa kumfanyia ukatili mwanafunzi wa darasa la saba.

Akitoa taarifa leo Septemba 3, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema watuhumiwa wanadaiwa kutumia mnyororo na kufuli, kumfunga mguu mwanafunzi wa darasa la saba, Hussein Juma (13), kwenye dawati na kisha kumfungia darasani Septemba Mosi, akidaiwa kuwa mtoro.

“Tunaendelea kukamilisha upelelezi wa tukio hilo, utakapokamilika taratibu nyingine za kisheria zitafuata,” amesema.

Mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Amina Juma amesema Septemba Mosi, saa nane mchana alikuja mlizi wa shule akidai mtoto huyo anahitajika shuleni kwa ajili ya maandalizi ya mitihani ya majaribio ya darasa la saba itakayofanyika kesho yake (Septemba 2).

“Nilimuambia mtoto anaumwa, anakohoa sana lakini alisisitiza anatakiwa shuleni, hivyo nilimuambia mtoto akaoge haraka aende. Nilimuomba mlinzi ahakikishe mtoto anarudi nyumbani mapema,” amesema na kuongeza:

“Waliondoka na mimi nikaendelea na kazi zangu, ilipofika saa moja usiku tunapigiwa simu na mlinzi kuwa mtoto amefungiwa ndani ya chumba kwa mnyororo na kufuli, hivyo tunatakiwa kumpelekea chakula na dawa maana anakohoa sana.”

Amesema aliwasiliana na mume wake, wakaenda shuleni walikomkuta amefungiwa ndani ya chumba hicho akiwa na mnyororo mguuni.

“Nilishangaa maana mtoto hajawahi kukosa shule zaidi ya siku mbili hizi ambazo alikuwa anaumwa kifua na nilimpeleka hospitali akapewa dawa. Hata juzi aliamka kujiandaa kwenda shuleni lakini hali yake ikawa siyo nikamshauri kubaki,” amesema.

Baba wa mtoto huyo, Juma Hassan amesema baada ya kupokea simu ya taarifa hizo alikwenda shuleni alikokuta geti limefungwa na hakuna mtu.

Amesema aliita jina la mtoto wake ndipo akaitika na kumtaka amfuate akieleza amefungwa kwenye dawati.

Ameiomba Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya mtuhumiwa akidai tukio la watoto kufanyiwa ukatili wa kufungiwa shuleni usiku kucha ni la kujirudia shuleni hapo.

Mwanafunzi huyo ameeleza alipochukuliwa nyumbani alipelekwa shuleni na kuamriwa kukaa kwenye dawati kisha alifungwa mnyororo akidaiwa kuwa mtoro kwa siku mbili.

“Nililetwa darasani nikaambiwa nikae, nashangaa mwalimu anakuja ananifunga akisema leo nitalinda shule na kesho nitafanya mitihani bila kupenda kisha akaondoka,” amedai mwanafunzi huyo.

Awali, mlinzi alisema ni mtoto wa pili kufungiwa ndani ya darasa kutokana na utoro.

Peter Richard, aliyeshuhudia tukio hilo amesema amesikitishwa na kitendo hicho kutekelezwa na mwalimu.