Mwanahabari mwingine afariki dunia Dodoma

Dodoma. Tasnia ya habari mkoani Dodoma imepata pigo lingine katika kipindi kifupi kufuatia kifo cha mwanahabari, Kadala Komba ambaye amefariki dunia leo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, alikokuwa amelazwa kwa matibabu.

Komba amefariki dunia ikiwa zimepita wiki mbili baada ya kifo cha Sharon Sauwa, mwanahabari mwandamizi aliyekuwa anatumikia vyombo vya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) mkoani Dodoma, kilichotokea Agosti 19, 2025.

Marehemu Kadala alikuwa miongoni mwa waandishi wenye ushawishi na uzoefu katika Mkoa wa Dodoma, akiwa ametoa mchango mkubwa katika sekta ya habari kupitia vyombo mbalimbali ikiwemo ABM Radio, Dar 24, Dodoma FM na Dodoma TV.

Hadi kifo chake, alikuwa anajitolea kama Ofisa Habari katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Taarifa za ugonjwa wa Kadala zilitolewa jana saa kumi jioni na mwandishi mwenzake, Rahim Shaaban, kupitia ujumbe mfupi wa maandishi katika kundi la viongozi wa Klabu ya Waandishi wa Mabari wa Mkoa wa Dodoma.

Shaaban alieleza kuwa Kadala alikuwa amelazwa katika wodi namba 11 na aliwahimiza waandishi wa habari kwenda hospitalini kumjulia hali.

Hata hivyo, ilipofika leo Jumatano Septemba 3, 2025 majira ya saa 3:07 asubuhi, Shaaban alituma ujumbe mwingine wa kifo cha Kadala Komba kwenye kundi sogozi hilo.

“Tanzia, taarifa ya msiba wa mwenzetu Kadala Komba amefariki asubuhi hii hospitali ya General,” ulieleza ujumbe huo.

Akitoa ratiba ya mazishi Katibu wa Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma (DPC), Blaya Moses amesema taarifa kutoka kwa familia ya Kadala Komba zinataarifu kuwa mwandishi huyo atazikwa mkoani Mbeya.

“Tangazo kwa mujibu wa taarifa ya familia dada yetu Kadala Komba atazikwa mjini Mbeya, mwili unatarajia kusafirishwa kesho saa 10 jioni kwenda Mbeya kwa sasa msiba upo Bahi nyumbani kwa marehemu,” ulitaarifu ujumbe huo.

Baada ya taarifa ya msiba kutolewa waandishi wa habari walionyesha majonzi yao kwa kumpoteza mwana tasnia mwenzao ambapo waliandika ujumbe wa kumtakia apumzike kwa amani.

Mwandishi wa habari wa TBC, Prisca Malekela aliandika, haki umeniliza ndugu yangu na kuona ‘dah hii life’ sio poa lala salama kipenzi tuonane baadaye, Mungu akurehemu huku mwandishi wa gazeti la Uhuru, Selina Mathew akiandika,  ‘Rest in Paradise’ Kadala, mbele yako nyuma yetu.

Felister Richard wa CFM ameandika jamani hatujapoa wewe dada umeondoka tena? Upumzike kwa amani.