Dar es Salaam. Wakati mradi wa mabasi yaendayo haraka awamu ya pili unaohusisha barabara ya Mbagala ukitarajiwa kuwa na mabasi 755, mgawanyo wake wa utoaji huduma utawahusu pia wakazi wa Buza na Kigamboni.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Septemba 3, 2025 na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart), Dk Athumani Kihamia, katika mahojiano na kituo cha runinga cha Clouds kuhusu maandalizi ya kuelekea kuanza kutoa huduma kwa mabasi hayo barabara ya Mbagala ifikapo Septemba 15, 2025.
Awali, huduma hizo zilikuwa zianze Septemba 1, 2025 lakini imeshindikana kutokana na kutokamilika kwa kituo cha kujazia gesi na kufungwa mageti janja yatakatumika kuchanjia kadi wakati wa kuingia kwenye vituo hivyo, lengo likiwa ni kuondokana na matumizi ya tiketi hali ambayo pia itasaidia uhifadhi wa mazingira na kudhibiti upotevu wa mapato.
Kutokana na hilo Dart pia imetumia fursa ya mahojiano hayo kuomba radhi wananachi kwa ucheleweshaji huo, huku ikieleza lengo ni kuhakikisha vitu vyote vinavyohitaji kabla ya mradi kuanza viwe vimekamilika kwa ufasaha.
Tayari kampuni ya Mofat itakayoendesha mabasi hayo imeshayaleta nchini mabasi hayo ambayo 99 yaliwasili Agosti 5, 2025 na mengine yaliletwa Agosti 26,2025 na tayari yapo katika karakana ya Mbagala Rangi Tatu huku mengine 42 yakitarajiwa kuletwa katikati ya mwezi huu na mpaka ikifika Oktoba kwa mujibu wa Mofat yote yatakuwa yameshawasili.
Magari hayo yenye urefu wa mita 18 kila moja yana uwezo wa kubeba abiria 160 na matarajio ya Mofat watakapoanza kutoa huduma ni kusafirisha abiria kuanzia 325,000 kwa siku hadi 400,000.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Dart kwa kushirikiana na taasisi zingine kuna jumla ya abiria 370,000 ambao husafiri kila siku kwa barabara ya Kimara huku kwa upande wa Mbagala wakiwa abiria 612,000 ikiwa ni zaidi ya mara mbili.
Moja ya swali aliloulizwa mtendaji huyo katika mahojiano hayo na mtangazaji, ni je wana uhakikia mabasi hayo yatawatosha wakazi wa Mbagala na kutahadharisha yasije yakajirudia yale ya changamoto za barabara ya Kimara.
Akifafanua hilo, Dk Kihamia amesema mabasi 255 ambayo yataletwa na kampuni ya Mofat, huku 151 yakiwa tayari yameshawasili nchini na kuhifadhiwa karakana ya Mbagala yatakuwa kwa ajili ya kutoa huduma barabara kuu.
Amezitaja barabara hizo kuwa ni Mbagala-Gerezani, Mbagala-Kivukoni na Mbagala-Morocco kupitia njia ya Magomeni Mikumi.
Wakati mabasi 500 kazi yake yatakuwa ni kuwatoa abiria kutoka maeneo ya pembezoni ikuhusisha Temeke, Chamazi, Buza na viunga vyake, lakini mengine yatawabeba abiria kutoka Toangoma, Kigamboni, Vikindu na kisha kuwaleta katika kituo kikuu cha Mbagala ambapo hapo wataunganisha safari zao kwenda maeneo mbalimbali katikati ya jiji. Kwa Kigamboni barabara watakayoitumia ni ile inayotarajiwa kujengwa hadi Vikindu.
“Hizo gari zitakazotoa huduma huko pembezoni tunaziita gari za njia mlishi (fider road), ambayo ukubwa wake ni mita 12 tofauti na mabasi haya ya barabara kuu ambayo yenyewe yana mita 18,” amesema.
“Pia, ieleweke idadi hii ya mabasi hatujayaleta kwa ajili ya kuangalia leo tu bali mpaka mwaka 2040, yaani hiyo idadi ya mabasi tumekadiria mpaka kizazi cha 2040 kwa sababu mkataba wake wa kuishi mabasi hayo ni miaka 12, hivyo katika kipindi hicho chote hatutaki kununua mabasi mengine,” amesema Dk Kihamia.
Aidha katika mgawanyo wa mabasi hayo 500, amesema kwa upande wa Kigamboni kutakuwa na mabasi 334 huku upande wa Temeke, Chamazi na Buza kutakuwa na mabasi 166 ambapo ukichanganya na yale ya Mofat 255 ndio yanaleta 755.
Tayari wawekezaji wawili wameshapitishwa wa kuleta mabasi hayo 500 kwa ajili ya njia mlishi ambao ni Metro City Link na YK link.
Yawaomba radhi wakazi wa Mbagala
Katika hatua nyingine Dk Kihamia alieleza sababu ya kuchelewa kufungwa kwa mageti huku mabasi yakiwahi na kueleza kuwa imetokana na mambo mbalimbali.
Mosi, amesema vyote viwili hutengenzwa na watu tofauti, hivyo huwezi kuagiza kimoja kabla ya kingine lakini kubwa viwanda vinavyotengeza ni tofauti na vyote havipo hapa nchini,.
“Kwa hiyo baada ya kiwanda cha mabasi kutengeneza na wakamaliza na wakawa wamepata ndege kwa haraka ndio mabasi yakaja, wakati ya mageti ikiwa yanasubiri meli ambapo hadi Septemba 8,2025 yatakuwa yamefika.Lakini pia hivi vitu (mageti na mabasi) sio kwamba ni vya kununua dukani ni vya kutengeneza na ni lazima visomane,” amesema Mtendaji huo.
Hata hivyo, ameeleza kuwa bado atasimamia msimamo wake kuwa ni vema kutengeneza vitu vya kudumu vya kuwaondelea adha ya muda mrefu, wananchi walikuwa wanaipitia katika usafiri kuliko kulipua kwa kuleta vitu ndani ya wiki moja ambavyo havitadumu kwa muda mrefu.
“Ni kutokana na hilo, ndio maana mwanzo wa mahojiano yangu nilitumia nafasi hii kuwaomba radhi wananchi wa Mbagala kutokana na kushindwa kuanza huduma kama tulivyowaahidi,” amesema.
Mtendaji huyo amesisitiza kuwa baada ya kukamilika kwa hatua hizo wakazi wa Mbagala suala la kero ya usafiri hawataliskia tena hata kwa kipindi cha miaka 50 ijayo na watasahau kabisa.