MWENGE WA UHURU KUPITIA MIRADI YA BILIONI 1.6 CHATO

Vyumba viwili vya madarasa shule ya msingi Nyabilezi

Shule ya Sekondari Kitela ikiwa ni miongoni mwa miradi itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru

Nyumba ya kulala wageni(The Grace Hotel) iliyopo kata ya Bwanga ambayo miongoni mwa miradi itakayowekewa jiwe la msingi na mwenge wa uhuru.

………..

JUMLA ya miradi yenye thamani ya shilingi Bilioni 1.6 inatarajiwa kutembelewa na mwenge wa uhuru wilayani Chato mkoani Geita kwa lengo la kuweka mawe ya msingi,kuzindua na kufungua miradi iliyotekelezwa na serikali kuu, halmashauri ya wilaya na wahisani wa maendeleo.

Mbali na miradi hiyo, pia mbio hizo zitaambatana na ugawaji wa mitungi 100 ya gesi kwa ajili ya kuchochea matumizi bora ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na uhifadhi wa mazingira.

Mkuu wa wilaya ya Chato Louis Peter Bura, amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari huku akisisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuupokea mwenge huo ambao utakuwa wilayani humo Septemba 3, 2025 kabla ya kukabidhiwa mkoani Kagera Septembe 7, 2025.

Kadhalika ameitaja miradi itakayo fikiwa na mwenge wa Uhuru kuwa ni uwekaji jiwe la msingi Zanahati ya Nyarututu, uwekaji jiwe la msingi The Grace Hotel iliyopo Bwanga, kuzindua mradi wa maji Minkoto, mradi wa usambazaji maji Minkoto, kutembelea chanzo cha maji msitu wa Silayo pamoja na upandaji miti, kutembelea mradi wa uwezeshaji vijana kiuchumi kijiji cha Rumasa, pamoja na uzinduzi wa daraja kwenye kijiji cha Mulanda.

Mingine ni Klabu ya wapinga rushwa shule ya Sekondari Mkungo, Ujumbe mahususi wa Mwenge wa Uhuru kwenye kijiji cha Musasa, kabla ya kuelekea shule ya msingi Nyabilezi kwaajili ya kuweka jiwe la msingi vyumba viwili vya madarasa, pamoja na uzinduzi wa shule mpya ya Sekondari Kitela iliyopo kata ya Chato na baadaye sherehe za mkesha wa Mwenge kwenye uwanja wa Ma Zaina.

Aidha Bura ametumia fursa hiyo kuwataka vijana kutambua thamani ya mwenge wa uhuru katika kuchochea maendeleo, amani na utulivu wa nchi na kwamba wasikubali kushawishiwa kwa namna yoyote ile kuchezea amani iliyopo nchini. 

Mtendaji wa kata ya Bwanga, Emanuel Mock pamoja na Ofisa maendeleo ya jamii kata hiyo, Nhabi Ndaki, wameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuhamasisha maendeleo kwa umma, ikiwemo ujenzi wa nyumba bora ya kulala wageni Bwangae ambayo itawekewa jiwe la msingi na mwenge wa uhuru na kwamba hatua hiyo itaongeza chachu ya uwekezaji katika wilaya ya Chato.

Kwa upande wake mkuu wa shule ya Sekondari Kitela, Erasto Michael na mtendaji wa kaya ya Chato, Mussa Nyanda, wamedai kuzinduliwa kwa baadhi ya miradi ya maendeleo pamoja na uwekaji wa mawe ya msingi utasaidia kupunguza changamoto zilizokuwepo awali katika jamii ikiwa ni pamoja na kuimalisha taaluma kwa wanafunzi ambao watapata miundo mbinu bora ya kujifunzia.

Hata hivyo mwenge huo wa uhuru utakimbizwa kwa umbali wa km 240 katika wilaya ya Chato kabla ya kukabidhiwa wilayani Muleba mkoani Kagera.