Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, amemwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mohamoud Thabit Kombo, ameshiriki kwenye maadhimisho ya miaka 80 ya Uhuru wa Vietnam yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam.
Mhe. Chumi ameipongeza Vietnam kwa kuadhimisha miaka 80 ya uhuru taifa hilo na miaka 60 ya ushirikiano mzuri uliopo wa Kidiplomasia na Tanzania.
Mhe. Chumi amesema maadhimisho hayo yanaakisi mafanikio makubwa yaliyopatikana kijamii na kiuchumi kutokana na kufanya kazi kwa biddii, ustahilivu, na kufanya mabadiliko. Kwa miaka 80 sasa Vietnam imejenga uchumi thabiti, imara, na maendeleo endelevu. Vietnam inalenga kufikia nchi iliyoendelea ifikapo mwaka 2045.
Tanzania na Vietnam zinashirikiana katika maeneo ya uwekezaji, biashara, elimu, afya, kilimo pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa miongo sita iliyopita.
Takwimu zinaonesha kuwa Vietnam ni nchi ya saba kwa kuwa soko kubwa la bidhaa za Tanzania ambapo mauzo ya bidhaa kutoka Tanzania kwenda Vietnam yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 226.6 mwaka 2020 hadi Dola milioni 314.2 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 38 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Kwa upande wake, Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Vu Thanh Huyen ameeleza dhamira ya Vietnam kuendeleza ushirikiano wa karibu na Tanzania, akisisitiza umuhimu wa kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo ya teknolojia kama njia ya kukuza uchumi wa mataifa yote mawili.
Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na Vietnam ulianza tangu mwaka 1965, na umefanikiwa kuimarisha ushirikiano wa uwili na wa kimataifa.













