Nangu, Yakoub wapata warithi jeshini

BAADA ya JKT Tanzania kutangaza kuachana na kipa Yakoub Suleiman na beki Wilson Nangu waliojiunga na Simba, kocha wa timu hiyo, Ahmad Ally amesema ameshapata mbadala wao.

Nangu na Yakoub wamesajiliwa Simba kila mmoja akisaini mkataba wa miaka mitatu, jambo ambalo Ally limemfurahisha akiona kwamba vijana wake wamewapa heshima kubwa JKT Tanzania.

Alisema katika nafasi ya Nangu tayari wamepatikana wachezaji wawili  Laurian Omar Makame aliyekuwa Fountain Gate na Paschal Mussa kutoka KMC anaoamini watafanya kazi nzuri msimu unaotarajia kuanza Septemba 17, ambapo siku moja kabla itapigwa mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga.

Kuhusu nafasi ya Yakoub, alisema tayari alishasajiliwa Ramadhan Chalamanda kutoka Kagera Sugar iliyoshuka daraja, lakini bado wanaendelea kusaka mwingine ili kujenga kikosi cha ushindani.

“Tupo katika mchakato wa kusajili kipa mwingine, kwani malengo yetu ni kumaliza ‘top 5’ tofauti na msimu uliopita tulishika nafasi ya sita na pointi 36 katika msimamo wa Ligi Kuu,” alisema kocha huyo na kuongeza:

“Mbali na hilo maandalizi yetu yanaendelea vizuri, tumerejea jijini Dar es Salaa Jumamosi kutokea Arusha ambako  tuliweka kambi ya wiki mbili.”

Msimu uliopita timu hiyo ilimaliza kwenye nafasi ya sita katikia msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 36 ikifunga mabao 27 na kuruhusu idadi hiyo katika michezo 30.