POLISI Kenya imeanza kwa kishindo michuano ya Kombe la Kagame 2025 kwa kuifumua Garde Cotes ya Djibouti kwa mabao 4-0, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Etienne Ndayiragije amesema kwa sasa hesabu zake amezielekeza kesho Ijumaa watakapoikabili Singida Black Stars ya Tanzania.
Mabingwa hao wa Kenya ambao watakashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, walianza kwa kishindo dhidi ya Wadjibouti juzi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na ni kama vile Ndayiragije amenogewa kwa kusema akili zao kwa sasa ni dhidi ya Singida aliokiri ni timu yenye wachezaji wenye viwango vya juu chini ya kocha Miguel Gamondi.
“Najivunia wachezaji wangu kwa kiwango kizuri ambacho walionyesha katika mchezo wetu wa kwanza, sasa ni wakati wa kuangalia mchezo ujao ambao naamini utakuwa na ushindani zaidi,” alisema kocha huyo wa zamani wa Mbao, Azam na KMC aliyewahi pia kuinoa Taifa Stars.
Ndayiragije anaifahamu Singida BS kama moja timu bora nchini hivyo alisema haitakuwa mechi nyepesi ukizingatia vijana hao wa Miguel Gamondi walianza mashindano hayo kwa sare dhidi ya Ethiopian Coffee.
Katika mechi za ufunguzi wa mashindano hayo ambazo zilichezwa juzi, alishuhudiwa kiungo mshambuliaji wa Polisi, Erick Zakayo ‘Di Maria’ akiweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao katika mashindano hayo.
Dakika 17 za kipindi cha kwanza zilitosha kwa Zakayo kuweka rekodi hiyo huku mabao mengine na Polisi yakifungwa na David Simiyu, Baraka Badi na Edward Omondi.
Msimu uliopita wa mashindano hayo, bao la kwanza lilifungwa ndani ya dakika nne tu, Mohammed wa El Hay Al-Wadi ya Sudan, alifunga dhidi ya JKU.
Mbali na rekodi ya bao la kwanza kwenye mashindano hayo katika mechi ya pili, alishuhudiwa kipa wa Ethiopian Coffee, Ibrahim Donald akionyeshwa kadi nyekundu ya kwanza na kuifanya timu yake kucheza zaidi ya dakika 30 za kipindi cha pili ikiwa pungufu uwanjani.