NRA yakatisha ‘Mobile Campaign’ kuwahi Kigoma, NLD ni kesho Tanga

Dar es Salaam. Wakati chama cha National League for Democracy (NLD) kitazindua kampeni zake kesho Septemba 4, 2025 mjini Tanga, chama cha National Reconstruction Alliance (NRA) kimelazimika kukatisha programu yake ya ‘mobile campaign’ leo Jumatano Septemba 3, 2025 ili kuwahi uzinduzi wa kampeni yao keshokutwa Ijumaa, Septemba 5, 2025 mjini Kigoma.

Tangu kuanza kwa kampeni, Agosti 28, 2025, NRA ambacho kwa mujibu wa ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kilikuwa kizindue kampeni zake siku hiyo mkoani Kigoma, hakikuzindua na badala yake kikaanza programu ya ‘mobile campaign’.

Programu hiyo ilianzia jijini Dar es Salaam kisha kuhamia mkoani Kilimanjaro kabla ya leo Jumatano Septemba 3, 2025 kupangwa kufanyika mkoani Pwani katika Wilaya za Bagamoyo na Kibaha.

Lengo la programu hiyo kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa NRA, Hassan Almasi, ni kuwapa mbinu za uchaguzi wagombea wake, kuzungumza nao ana kwa ana na kuwa tayari kwa kampeni, sanjari na kuzungumza na wananchi kwa karibu zaidi kabla ya kuanza kuinadi ilani na sera za chama hicho kuomba ridhaa kwa wananchi.

Hata hivyo, leo saa 6 mchana, chama hicho kimelazimika kusitisha utaratibu huo kwa kile ambacho Almasi amebainisha ni kuwahi kuweka mambo sawa mkoani Kigoma ambako wanakwenda kuzindua kampeni zao Ijumaa.

“Tumefanya mobile campaign Dar es Salaam na Kilimanjaro, leo ilipaswa tuwe Pwani katika maeneo ya Msata, kisha Chalinze, Mlandizi, Miembe Saba, Mwendapole na kumalizikia Loliondo Sokoni, kisha tulipaswa kufanya kikao cha ndani hapo Kibaha.

“Hata hivyo, tumesitisha zoezi hilo na kuanza kuelekea Kigoma kwenda kuweka mambo sawa tayari kwa uzinduzi wa kampeni zetu kule,” amesema na kuongeza:

“Tumeona logistics (mipango) haijakaa sawa, kwa kuwa tulikuwa Kilimanjaro, hivyo tukasitisha mobile campaign,” amesema.

Chama hicho leo Septemba 3, kwa mujibu wa ratiba ya INEC, kilipaswa kuendelea na kampeni mkoani Kigoma katika kata zote za Wilaya ya Kasulu na Buhigwe, kwa mgombea wake wa urais na mgombea mwenza kuwa katika Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma.

Almasi amesema wamepangua ratiba hiyo, akisisitiza katika mikoa yote walipotakiwa kufanya kampeni tangu Agosti 28, itakapotoka ratiba ya awamu ya pili ya Oktoba, wataifidia na yote watafika.

Mikoa hiyo ni Mtwara, Tanga, Ruvuma, Dar es Salaam, Mbeya, Kaskazini Pemba, Iringa, Morogoro na Kagera.

Mbali na NRA, chama cha NLD kesho kitazindua kampeni zao mjini Tanga, ambapo kwa mujibu wa mgombea wa nafasi ya urais, Doyo Hassan Doyo, wanakwenda kuanisha vipaumbele na ilani ya chama chao katika tukio hilo kubwa.

“Tumejipanga kufanya uzinduzi wa kishindo kwenye stendi ya Pangani, wananchi wajitokeze kwa wingi kusikiliza sera na ilani yetu na kutupa ridhaa ya kuwatumikia,” amesema.

Kwa upande wa ADC chenyewe kinatarajiwa kuzindua kampeni zake Septemba 7, 2025 jijini Mwanza,  wakati Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Chama cha Wakulima (AAFP), Chama cha Wananchi (CUF), Demokrasia Makini na chama cha CCK vikiwa tayari vimeshazindua kampeni zao.