Nyaishozi Mfano wa shule Bora zinazotangaza ushirika kielimu

Na Diana Byera,Karagwe

Wamiliki wa shule binafsi wilayani Karagwe, mkoani Kagera, wametakiwa kuzingatia lengo kuu la kuanzisha shule,ambalo ni kutoa huduma ya elimu badala ya kuzigeuza shule hizo kuwa chanzo cha biashara na faida kubwa.

 Wito huo umetolewa kufuatia ongezeko la malalamiko kutoka kwa jamii kuhusu gharama kubwa na michango mingi isiyoelezeka katika baadhi ya shule binafsi.

Akizungumza katika mkutano uliohusisha wazazi, walezi, wakuu wa shule, waratibu wa elimu na wamiliki wa shule katika viwanja vya shule ya sekondari ya Nyaishozi, Mdhibiti wa Ubora wa Elimu Wilaya ya Karagwe, Higmagway Hermani, alisema kuwa baadhi ya shule binafsi zimepoteza mwelekeo wa awali wa utoaji huduma kwa jamii na badala yake zimejikita katika mtazamo wa kibiashara.

“Lengo la serikali kuruhusu shule binafsi lilikuwa ni kuongeza wigo wa upatikanaji wa elimu kwa watoto wote, Hata hivyo, hivi karibuni baadhi ya shule zimekuwa na hulka ya kibiashara, hali inayowavunja moyo wazazi wenye kipato cha chini ni muhimu kwa wamiliki wa shule kuangalia upya dira zao na kupunguza gharama, ili kila mtoto apate haki yake ya msingi ya elimu.”alisema Herman 

Hermani alitoa mfano wa Shule ya Wakulima ya Nyaishozi, kama miongoni mwa shule binafsi zinazotoa huduma bora kwa gharama nafuu ambapo Shule hiyo ilianzishwa na wakulima wa kahawa wa wilaya ya Karagwe  na Kyerwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wa wakulima wanapata elimu bora kupitia mfumo wa uchangiaji unaozingatia uwezo wa familia zao.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Bodi  wa shule Hiyo  Fidoline  Kasenene, alisema  michango ya wanafunzi hukatwa kidogo kidogo kutoka kwenye mapato ya zao la kahawa, badala ya kuwatwika wanafunzi au wazazi mzigo wa ada kubwa ya moja kwa moja na hakuna mtoto anayepaswa kusumbuliwa 

Naye Enikia Bisanda, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Kagera, alisema shule hiyo ni mfano wa kuigwa kwani inawajengea wanafunzi maarifa ya ushirika na namna ya kutumia elimu hiyo kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo.

“Watoto wa wakulima wanaohitimu kutoka shule hii wana uelewa mpana juu ya ushirika na kilimo cha kisasa. Tunawahimiza wahitimu kutumia elimu waliyoipata kuleta mabadiliko chanya katika vijiji na familia zao,” alisema Bisanda.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Audax Gereon, alisema shule ya Nyaishozi inajivunia kuwa na mtaala wa kipekee unaolenga kumwandaa mwanafunzi katika maisha halisi, hasa kupitia somo la Kilimo kwa Vitendo, ambalo ni la lazima kwa wanafunzi wote.

“Shule yetu inawafundisha watoto si tu kwa nadharia, bali pia kwa vitendo, Lengo ni kuwapa maarifa ya moja kwa moja yatakayowawezesha kubadilisha maisha yao na ya jamii zao, Kwa sasa tumeanzisha mchepuo wa sayansi kwa kidato cha tano na sita, ili kuandaa wataalamu wa baadaye wa kilimo na sayansi. Alisema Gereoni

mwenyekiti wa chama kikuu Cha Ushirika Kinachojihusisha Na zao la Kahawa Kwa Karagwe na Kyerwa KDCU  Faxson Josiha  alisema shule ya Nyaishozi ni mfano halisi wa jinsi elimu inavyoweza kutolewa kama huduma muhimu kwa jamii, si kama biashara  na kudai kuwa wamiliki wa shule binafsi kote nchini wanaweza kuanza  kutafakari upya nafasi yao katika ujenzi wa taifa kupitia elimu jumuishi na nafuu.