Nyenzo utekelezaji sera ya maendeelo watoto yapatikana

Unguja. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeida Rashid Abdallah amesema kuwa mpango jumuishi wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto wa miaka mitano, ni nyenzo katika utekelezaji wa sera za maendeleo ya watoto pamoja na kufanikisha malengo ya kitaifa na kimataifa.

Kauli hiyo ameitoa alipokuwa akifungua kikao cha kazi ambacho kinafanyika Septemba 3, 2025, katika Kijiji cha Jambiani, Unguja.

Kikao hicho kimelenga kuandaa mpango huo na kimepangwa na Taasisi ya Ofisi ya Rais ya Ufuatiliaji wa Utendaji Serikalini Zanzibar (ZPDB).

Abdallah ameongeza kuwa mpango huu unahimiza utoaji wa huduma bora za afya, chanjo, lishe bora, ulinzi wa mtoto pamoja na malezi yenye mwitikio.

“Hii itachangia moja kwa moja katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan lengo namba nne linalolenga kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano.

“Programu hii ni muhimu sana kwa kuwa inajikita katika kuhakikisha kila mtoto wa Kizanzibari anapata malezi bora, afya njema, lishe inayostahiki, ulinzi, na fursa ya kujifunza katika hatua za awali za maisha yake,” amesema Abeida.

Naye Naibu Katibu Mkuu Taaluma, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Dk Mwanakhamis Adam Ameir amesema Zanzibar kuna baadhi ya watoto wa darasa la tatu mpaka la saba hawajui kuandika kutokana na kukosa fursa ya kuijifunza katika umri wa awali.

Wizara hiyo pia inafanya jitihada ya kuwafundisha walimu kuhusu malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto hasa katika ulaji kwani baadhi ya vyakula vinavyouzwa katika mashuleni siyo salama ikiwemo malai.

Ameeleza kwamba elimu kuhusu malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto imeanzishwa katika Chuo cha Ualimu Nkuruma, wanafunzi wa kidato cha nne na sita waliopata daraja la kwanza na pili wanafundishwa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ili waweze kuwalea watoto katika misingi inayohitajika.

Naibu Mkurugenzi kinga Wizara ya Afya, Dk Fatma Kabole amesema changamoto ya afya ya akili kwa akinamama inaongezeka lakini jitihada zinazofanywa zimesaidia kuboresha huduma za afya kwa kujenga hosipitali na kuimarisha vituo vya afya.

Akizungumza katika kikao kazi hicho, Mtalaamu wa Hifadhi ya Mtoto kutoka Shirika la Kuhududmia Watoto Duniani (Unicef), Ahmed Rashid Ali amesema kuna umuhimu kuwekeza katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwani faida yake ni sawa na kuwekeza shilingi moja katika biashara na kupata faida ya shilingi saba.

Amesema utafiti umeonesha asilimia 18 watoto wamedumaa huku asilimia 40 hawakufikia viwango vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali, hivyo Shirika la Unicef linashirikiana na Serikali kupata kinga na matibabu ya changamoto iliyopo.

Mapema akizungumza Mratibu wa Programu ya Malezi, Makuzi na maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka ZPDB, Dk Maryam Issa amesema lengo la programu hiyo ni kuhakikisha watoto 276,000 wa Zanzibar wanakuwa katika mwelekeo unaofaa kwa kuhakikisha wanapata huduma za afya, lishe, ulinzi na usalama wa mtoto ifikapo 2030.

Amesema shughuli mbalimbali zimekuwa zikitekelezwa kupitia programu hiyo ikiwemo kufanya utafiti wa hali ya malezi na makuzi ya awali ya mtoto ya Zanzibar (ECD base line survey), ambapo miongoni mwa matokeo ya utafiti huo yameonesha kwamba takribani asilimia 32 ya watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 3 Zanzibar wamechelewa kimaendeleo.

Pia, Dk Maryam amesema programu hiyo imefanya  utafiti mdogo wa kuangalia huduma rafiki za Malezi na makuzi ya mtoto katika masoko, hospitali na shule za maandalizi, hali ambayo inaonesha huduma hizo  hazipo, hivyo programu inakwenda kuweka huduma hizo katika maeneo hayo.

Maandalizi ya Mtalaa wa Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii yamekamilika. Sasa tayari mafunzo kwa wahudumu hao wa afya yameanza katika maeneo ya Unguja na hatua inayofuata wanatarajia kwenda kisiwani Pemba kutekeleza.

Ofisa Mwandamizi kutoka wizara ya Kilimo, Umwagiliaji Maliasili na Mifugo amesema wizara hiyo inazalisha asilimia 60 ya vyakula vya mbogamboga, protini, vitamini lakini shida iliyopo ni katika uelewa wa matumizi kwani tatizo lipo kwa wenye watu wenye uwezo na wasiokuwa na uwezo hivyo elimu ya lishe inahitajika kwa jamii.