Dar es Salaam. Ahueni inaendelea kushuhudiwa kwa watumiaji wa vyombo vya moto nchini baada ya bei za petroli na dizeli kuendelea kushuka kwa mwezi wa tano mfululizo huku watumiaji wa mafuta ya taa wakiugulia maumivu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei kikomo za mafuta zinazotumika kuanzia leo Jumatano Septemba 3, 2025, zinaonesha kupungua kwa kwa Sh36 kwenye petroli na Sh23 kwenye dizeli kwa mafuta yaliyopokewa Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara mtawalia.
Kuendelea kushuka kwa mafuta kunachangia na bei ya soko la dunia, gharama za ubadilishaji fedha kupungua.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Andilile bei ya petroli katika soko la dunia imepungua kwa asilimia 0.2, dizeli kwa asilimia 5.5 na mafuta ya taa kwa 3.5.
Pia, kwa bei za Septemba, 2025, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni umepungua kwa 3.96.
“Hata hivyo, gharama za kuagiza mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 20.73 kwa mafuta ya petroli, asilimia 7.75 dizeli na asilimia 2.62 kwa mafuta ya taa, katika Bandari ya Mtwara hakuna mabadiliko na kwa Bandari ya Tanga zimepungua kwa asilimia 12.66 kwa mafuta ya petroli na asilimia 12.66 kwa dizeli,” imesema taarifa hiyo.
Hiyo ikiwa na maana kuwa sasa lita moja ya mafuta inayopitia katika Bandari ya Dar es Salaam itauzwa kwa Sh2,807 kutoka Sh2,843 iliyotumika Agosti mwaka huu, dizeli itanunuliwa kwa Sh2,754 kutoka Sh2,777.
Hata hivyo, kwa watumiaji wa mafuta ya taa yanayopitia katika bandari hiyo watalazimika kutumia fedha Zaidi kwani lita moja sasa itauzwa kwa Sh2,774 kutoka Sh2,768 iliyokuwapo Agosti mwaka huu.
Kwa wanunuaji wa rejareja kwa mafuta yanayopita Bandari ya Tanga sasa watanunua petroli lita moja kwa Sh 2,868 kutoka Sh2, 904 iliyokuwapo Agosti mwaka huu, dizeli Sh2,816 kutoka Sh2,839 huku mafuta ya taa yakiongezeka hadi Sh2,835 kutoka Sh2,829, mtawalia.
Kwa Bandari ya Mtwara, petroli sasa itanunuliwa Sh2,899 kutoka Sh2,935, dizeli Sh2,847 badala ya Sh3,020 na mafuta ya taa yakiongezeka hasi Sh 2,866 kutoka Sh2,86.
Ewura inabainisha kuwa katika upande wa bei za mwezi Septemba 2025, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni umepungua kwa asilimia 3.96.
Kufuatia hilo, wameendelea kuvitaka vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.
“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,” imesema taarifa hiyo.
Pia, imewataka wauzaji wa mafuta Wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.